1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaNiger

ECOWAS waamua kujizuia kuingilia kati kijeshi Niger

11 Agosti 2023

Jumuiya ya kiuchumi ya nchi za Afrika Magharibi yaamua kuchukuwa mwelekeo wa kidiplomasia zaidi na kujizuia kuingilia kijeshi mgogoro wa Niger kuuondowa utawala wa kijeshi.

Rais wa Ivory Coast Alassane Ouattara akiwa na Mwenyekiti wa tume ya ECOWAS Omar Touray
Rais wa Ivory Coast Alassane Ouattara (Kulia) akikutana na Rais wa tume ya ECOWAS Omar TourayPicha: KOLA SULAIMON/AFP

Viongozi wakuu wa nchi wanachama wa Jumuiya ya kiuchumi ya nchi za Afrika Magharibi, ECOWAS wamesema watafuata njia ya mazungumzo na viongozi wa kijeshi waliotwaa madaraka kwa nguvu nchini Niger.

Uamuzi huo umechukuliwa kwenye mkutano wa kilele uliofanyika mjini Abuja huko Nigeria.

Viongozi wakuu wa ECOWAS wamesema mazungumzo ndiyo yatakayokuwa msingi wao mkubwa katika juhudi za kuutafutia ufumbuzi mgogoro wa Niger na kuonekana kuweka pembeni kitisho cha kuingilia kijeshi kurudisha utawala wa kidemokrasia nchini humo.

Kikao cha ECOWAS kilichofanyika mjini Abuja, NigeriaPicha: Kola Sulaimon/AFP/Getty Images

Rais wa Nigeria ambaye ndiye mwenyekiti wa sasa wa jumuiya hiyo Bola Tinubu anaongoza mkutano huo wa kilele mjini Abuja na tayari ameshasema ni muhimu kutanguliza mbele mazungumzo ya kidiplomasia na mwelekeo wa kufanya mdahalo.

Kiongozi huyo wa Nigeria amesema, "Leo tumekutana tukiwa kwenye hali ya dharura kubwa na azma thabiti iliyotokana na ahadi tulizotowa wakati wa mkutano wetu wa mwanzo wa kilele, kuhusu mgogoro wa kisiasa unaoikumba nchi ndugu yetu. Wakati wa mkutano huo wa mwanzo tulipaza sauti za mshikamano wetu na watu wa Niger na serikali yao iliyochaguliwa kidemokrasia ya muheshimiwa rais Mohammed Bazoum, kwa kulaani hatua ya jeshi ya kutwaa kwa nguvu madaraka na kuwashikilia kwa njia zisizokuwa halali rais na maafisa wengine.''

Jeshi Niger labaki na msimamo mmoja

Juu ya hilo rais huyo wa Nigeria amekiri kwamba licha ya kikao chao cha mwanzo kutowa muda wa siku saba wa kutaka kurudishwa madarakani rais Bazoum, jeshi nchini Niger limeendelea kukataa kufanya hivyo na linamshikilia rais huyo pamoja na familia yake katika ikulu ya rais mjini Niamey na maafisa wengine.

Soma pia: ECOWAS bado inatumai kuna fursa ya upatanishi Niger

Rais wa Nigeria Bola Ahmed TinubuPicha: Kola Sulaimon/AFP/Getty Images

ECOWAS ilitowa muda wa hadi Jumapili iliyopita kurudishwa madarakani rais Mohammed Bazoum baada ya jeshi kufanya mapinduzi Julai 26.

Tinubu kama mwenyekiti wa jumuiya hiyo ya maendeleo ya nchi za Magharibi mwa Afrika, amesema wanabidi kuzihusisha pande zote zinazohusika kwenye mgogoro wa Niger wakiwemo viongozi wa kijeshi katika mazungumzo ya uwazi ili kuwashawishi kuachia madaraka na kumrudisha rais halali.

Kadhalika ametilia mkazo kwamba ni jukumu lao kutumia njia zote za kuwaleta pamoja kuhakikisha namna bora ya kurudisha utawala wa kikatiba katika nchi hiyo.

ECOWAS haina sauti moja kuhusu kuingia kijeshi Niger

Mpaka sasa kitisho cha uingiliaji kati wa kijeshi kwenye mgogoro huu kimeonesha kuwa suala linaloleta mgawanyiko miongoni mwa wanachama wa ECOWAS na mataifa mengine ya Afrika yana wasiwasi kuhusu kuongezeka mgogoro utakaoleta madhara yasiyoweza kutabirika.

Jenerali Mohamed Toumba wa NigerPicha: Balima Boureima/AA/picture alliance

Hata hivyo wachambuzi wanasema jumuiya hiyo huenda haina tena chaguo kutokana na suala la uingiliaji kijeshi kukosa uungwaji mkono.

Soma pia: ECOWAS kuwawekea vikwazo watawala wa kijeshi Niger

Mkutano wa Abuja uliofanyika faragha umehudhuriwa na viongozi wakuu 9 kati ya 11 waliotarajiwa kushiriki wakiwemo marais wa Senegal, Ivory Coast, Ghana, Togo, Benin, Guinea Bissau na Sierra Leone.

Mkutano huo pia ulihudhuriwa na viongozi wasiokuwa wanachama wa ECOWAS, kutoka Mauritania na Burundi.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW