1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaNiger

ECOWAS yakubaliana uwezekano wa kuingilia kati Niger

Sylvia Mwehozi
5 Agosti 2023

Wakuu wa majeshi wa Jumuiya ya kikanda ya Afrika Magharibi ya ECOWAS wamekubaliana juu ya mpango wa uwezekano wa kuingilia kati kijeshi nchini Niger, baada ya viongozi wa mapinduzi kushindwa kurejesha utawala wa kiraia.

Nigeria, Abuja | ECOWAS-Mgogoro wa Niger
Wakuu wa ulinzi wa Jumuiya ya ECOWAS katika mkutano wao AbujaPicha: Kola Sulaimon/AFP/Getty Images

Wakuu wa majeshi wa Jumuiya ya ECOWAS walikutana kwa mazungumzo katika mji mkuu wa Nigeria wa Abuja, kujadili njia za kushughulikia mgogoro huo, ambao ni wa hivi karibuni katika mkururo wa mapinduzi ya kijeshi kuikumba kanda ya Sahel tangu mwaka 2020. Kamishna wa ECOWAS Abdel-Fatau Musah amesema kuwa "vipengele vyote vya uwezekano wa uingiliaji kati vimefanyiwa kazi"

Soma pia:Jumuiya ya ECOWAS inaweza kuziwajibisha tawala za kijeshi?

Vipengele hivyo vinajumuisha "rasilimali zinazohitajika, namna gani na lini" wanaweza kutuma wanajeshi. Musah ameongeza kuwa Jumuiya hiyo ya kikanda inataka "diplomasia kufanya kazi" na kusema wanatuma ujumbe wa wazi kwa viongozi wa kijeshi kwamba wanawapatia fursa zote za kubatilisha kile walichokifanya.

ECOWAS ilisema Jumapili iliyopita kwamba inawapatia wiki moja viongozi wa mapinduzi kumrejesha madarakani Rais aliyechaguliwa kidemokrasia Mohamed Bazoum, la sivyo watakabiliwa na uwezekano wa uingiliaji kati kinguvu.

Viongozi wa kijeshi wa Niger wameonya kwamba jaribio lolote la kuingilia kati nchi hiyo litakabiliwa na upinzani. Mali na Burkina Faso ambako pia wanajeshi walifanya mapinduzi tangu 2020, nazo pia zimeungana na jirani yake zikionya kuwa uingiliaji wowote wa kikanda utakuwa ni tangazo la vita dhidi yao.

Kamishna wa masuala ya siasa, usalama na uchumi wa ECOWAS Abdel-Fatau Musah(katikati)Picha: KOLA SULAIMON/AFP

Urusi ambayo ushawishi wake unaongezeka kwenye kanda hiyo, imetaja hatua hizo kwamba sio suluhu ya mgogoro. Nchi jirani ya Benin na Ujerumani zimehimiza njia za kidiplomasia kushughulikia mzozo wa Niger.

Ujumbe wa ECOWAS uliwasili mjini Niameysiku ya Alhamis, lakini haukufanikiwa kukutana na kiongozi wa mapinduzi Abdourahamane Tiani wala rais Bazoum.

Katika hatua nyingine ambapo mgogoro huo umezidi kutokota, viongozi wa kijeshi wa Niger walitangaza Ijumaa kuvunja ushirikiano wa kijeshi na Ufaransa, wakimwelezea mkoloni wake huyo wa zamani kuwa na "mtizamo wa kutojali" na jinsi ilivyoshughulikia hali hiyo. Ufaransa imekataa tangazo hilo ikisisitiza kwamba "serikali halali ndio inaweza kuamua”.

Niger imekuwa na mchango muhimu katika mapambano dhidi ya wapiganaji wenye itikadi kali kwenye kanda ya Sahel tangu 2012, huu Ufaransa na Marekani zikiwapeleka wanajeshi wapatao 2,500 katika nchi hiyo.

Kumekuwa na hali ya upinzani dhidi ya Ufaransa katika kanda ya Sahel huku ushawishi wa Urusi ukiongezeka kupitia kundi lake la mamluki la Wagner. Katika inayoashiria kurejea kwa hali ya kawaida, viongozi wa mapinduzi wameaondoa marufuku ya kutoka nje usiku tangu mapinduzi.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW