ECOWAS yatoa wito wa umoja kwa nchi za Afrika Magharibi
9 Februari 2024Jumuiya ya Kiuchumi ya Mataifa ya Afrika Magharibi ECOWAS imefanya mkutano wa dharura na kujadili masuala muhimu yanayoikumba kanda hiyo, ikiwa ni pamoja na hatua ya nchi za Mali, Burkina Faso na Niger kujiondoa katika umoja huo pamoja na mzozo wa kisiasa unaoendelea nchini Senegal baada ya uchaguzi mkuu kuahirishwa.
Yusuf Maitama Tuggar ameeleza kwamba kujiondoa kwa nchi hizo, kutasababisha matatizo yatakayoleta madhara zaidi kwa raia wa kawaida.
Maitama Tuggar ameyasema hayo katika mji mkuu wa Nigeria Abuja, kulikofanyika mkutano huo wa mawaziri wa mambo ya nje na ulinzi wa jumuiya hiyo ya Afrika Magharibi.
Soma pia:ECOWAS kudhoofika baada ya wanachama wake watatu kujiondoa?
Hata hivyo, Burkina Faso, Mali, Niger na Guinea, ambao wote walichukuliwa hatua ya kusimamishwa kwenye jumuiya ya ECOWAS kufuatia mapinduzi ya kijeshi, hawakutuma wawakilishi wao katika mkutano huo.
Rais wa Halmashauri Kuu ya ECOWAS Omar Alieu Touray amehimiza pia umoja akisema huu ni wakati ambao wanachama wa ECOWAS wanahitaji kushikamana huku akikumbushia pia misingi ya jumuiya hiyo.
"Sidhani ni ari na mapenzi ya watu wa jumuiya ya ECOWAS kuachana na kanuni za kidemokrasia, kuachana na uwazi na kuachana na ushiriki jumuifu katika utawala."
Touray, amesema uamuzi wa ghafla wa nchi hizo tatu kutangaza kujiondoa, haukufuata masharti yaliyowekwa na Jumuiya hiyo, yanayoamuru kuwa taifa linalotaka kujiondoa linapaswa kuwasilisha barua mwaka mmoja kabla ya hatua hiyo.
Mazungumzo ya faragha na mjadala kuhusu mzozo wa Senegal
Wajumbe wa baraza hilo la usuluhishi na usalama la ECOWAS walifanya mazungumzo ya faragha kwa zaidi ya saa sita kabla ya kurejea na kuhitimisha kikao hicho bila hata hivyo kutoa taarifa iliyo wazi juu ya hatua gani ambazo zingelichukuliwa.
Burkina Faso, Mali na Niger zilitangaza mwezi uliopita hatua yao ya pamoja ya kujiondoa kwenye ECOWAS, na hivyo kuzusha matatizo ya kidiplomasia kwa jumuiya hiyo iliyokuwa na jumla ya nchi 15 wanachama.
Wajumbe wa Baraza hilo walijadili pia mzozo wa kisiasa nchini Senegal kufuatia hatua ya kuahirishwa uchaguzi wa rais kwa miezi kumi, jambo ambalo limezusha maandamano ya umma na hofu ya kuzuka machafuko.
Soma pia: Umoja wa Afrika wasema "umefadhishwa" na kujiondoa Niger, Mali na burkina Fasso ndani ya ECOWAS
Siku ya Jumanne, ECOWAS iliitahadharisha Senegal dhidi ya kuhatarisha "amani na utulivu" hasa nyakati hizi ngumu kwa eneo la Afrika Magharibi, lakini hadi sasa haifahamiki ni hatua gani itakayochukuliwa na jumuiya hiyo ikiwa rais wa Senegal Macky Sall atakaidi onyo hilo.
Kikao kisicho cha kawaida cha Jumuiya ya Kiuchumi ya Afrika Magharibi (ECOWAS) pia kilizungumzia uamuzi wa Rais Macky Sall wa kuchelewesha uchaguzi nchini Senegal, wasiwasi mkubwa kwa eneo hilo ambao ulikuja wiki moja tu baada ya Burkina Faso, Mali na Niger kutangaza kuondoka.