1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaEcuador

Ecuador: Daniel Noboa ashinda uchaguzi wa rais

16 Oktoba 2023

Mfanyabiashara huyo wa chama cha mrengo wa kati-kulia, mwenye umri wa miaka 35, atakuwa rais wa kwanza mwenye umri mdogo zaidi Ecuador. Lakini anakabiliwa na changamoto kubwa.

Daniel Noboa mwenye umri wa miaka 35 ndiye rais mteule mwenye umri mdogo zaidi Ecuador.
Daniel Noboa mwenye umri wa miaka 35 ndiye rais mteule mwenye umri mdogo zaidi Ecuador.Picha: Martin Mejia/AP/picture alliance

Baada ya asilimia 93 ya kura kuhesabiwa, Noboa alikuwa mbele kwa asilimia 52 huku Gonzalez akiwa wa pili kwa asilimia 48.

Gonzalez amekubali kushindwa na amempongeza Noboa kwa ushindi wake mnamo wakati akipanga kumpigia simu. Amesema hayo alipokuwa akizungumza na wafuasi wake mjini Quito.

Wagombea hao wawili walishiriki kura ya marudio baada ya kuchukua nafasi ya kwanza na pili mbele ya wagombea wengine sita katika duru ya kwanza ya uchaguziwa Agosti 22.

Masuala makuu ambayo yanawapa wapiga kura changamoto nchini humo ni pamoja na uchumi ambao umetatizika tangu kutokea kwa janga la COVID-19, ongezeko la uhalifu ikiwemo mauaji na ghasia za magerezani.

Uchaguzi huo wa Jumapili ulifanyika bila ya matatizo makubwa.

"Leo Equador imeshinda, demokrasia imeshinda,” alisema Diana Atamint ambaye ni rais wa Baraza la Taifa la Uchaguzi nchini humo.

Uchaguzi huo wa mapema uliitishwa baada ya rais kuvunja bunge mwezi Mei

Uchaguzi wa Equador ulifanyika mapema baada ya Rais Guillermo Lasso kuvunja bunge mnamo mwezi Mei, ili kuepusha kura ya kutokuwa na imani dhidi yake, miaka miwili tu baada ya kuchaguliwa kwake.

Noboa ataongoza kwa muda wa mwaka mmoja na nusu au hadi 2025, kipindi kilichobakia cha muhula ambao wake Lasso

Upigaji kura ni jambo la lazima kwa raia wote wa kati ya umri wa miaka 18 hadi 64. Jumla ya watu milioni 13 nchini humo wanastahiki kupiga kura. Wale ambao hawafuati sheria hiyo hupigwa faini ya takriban dola 45.

Luisa Gonzalez mwenye umri wa miaka 45, wa chama cha mrengo wa kushoto ‘Citizen Revolution' alichaguliwa na Rais Rafael Correa kuwania urais

Wakati wa utawala wa Rais Rafael Correa, Gonzalez alishikilia nyadhifa mbalimbali serikalini, na alikuwa mbunge hadi Mei, 2023.

Mwanzoni mwa kampeni, alisema Correa atakuwa mshauri wake, lakini hivi karibuni amekuwa ajijaribu kujitenga na Correa huku akiwasogelea karibu wafuasi wanaompinga rais huyo wa zamani.

Luisa Gonzalez akiwa kwenye mojawapo ya mikutano ya kampeni mjini Quito Agosti 20 katika kinyang'anyiro cha kuwania urais nchini Ecuador.Picha: Franklin Jacome/Getty Images

Noboa, mrithi wa milki ya ndizi

Noboa mwenye umri wa miaka 35, ni mrithi wa mali iliyojengwa kutokana na zao kuu la Ecuador, ndizi. Baba yake aliyewahi kugombea urais mara tano bila kushinda, anaendesha kampuni kubwa ya ndizi.

Maisha ya kisiasa ya Daniel Noboa yalianza mwaka 2021 aliposhinda kiti cha ubunge nchini humo na akawa mwenyekiti wa Tume ya Maendeleo ya Kiuchumi.

Kabla ya hapo, Daniel Noboa alishikilia nyadhifa mbalimbali za usimamizi katika sekta ya usafirishaji na biashara katika kampuni ya baba yake Noboa Corp.

Raia wa Equador walipiga kura dhidi ya hali ya nyuma ya machafuko ambayo yameongezeka katika miaka michache iliyopita.

Aliyekuwa mgombea mkuu wa urais Fernando Villavicencio, anayefahamika kutokana na msimamo wake mkali dhidi ya ufisadi, aliuawa katika mkutano wa kampeni mwezi Agosti, siku chache tu kabla ya duru ya kwanza ya uchaguzi.

Guillermo Lasso, rais anayeondoka madarakani Ecuador.Picha: Juan Diego Montenegro/dpa/picture alliance

Watuhumiwa mauaji ya mgombea Urais Ecuador wauwawa gerezani

Ongezeko la uvunjifu sheria Equador

Hali ya kutii sheria nchini Equador ilizorota wakati wa utawala wa Lasso. Viwango vya mauaji viliongezeka mara nne katika miaka miwili tu, na kubadilisha hali kuwa ya vurugu

Ripoti na habari kuhusu ongezeko la uhalifu, ghasia na mauajindani na nje ya magereza zilidhoofisha imani ya raia kwa serikali.

Lasso alijitahidi kudhibiti mizozo kati ya mashirika ya ulanguzi mihadarati yaliyokuwa yakipigania udhibiti wa bandari za Ecuador ambazo ni njia muhimu katika kusafirisha mihadarati kutoka Colombia na Peru hadi Marekani na Ulaya.

Kutanuka kwa uhalifu wa kupangwa kulihatarisha idara ya mahakama na hivyo kudhuru zaidi sifa ya Lasso.

Chini ya utawala wa Lasso, vifo kutokana na ghasia viliongezeka hadi kufikia 4, 600 mwaka 2022, hiyo ikiwa idadi ya juu zaidi katika historia ya taifa hilo dogo la Amerika ya Kusini.

Kulingana na takwimu ya polisi nchini humo, katika nusu ya kwanza ya mwaka 2023, watu 3, 568 walikuwa wameuawa kutokana na vurugu.

rm/msh (AP, Reuters, dpa)

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW