1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaEcuador

Ecuador: Mgombea urais auawa kwa kupigwa risasi

10 Agosti 2023

Mgombea urais nchini Ecuador Fernando Villavicencio ameuawa hapo jana kwa kupigwa risasi na mtu asiyejulikana wakati akiwa kwenye kampeni za uchaguzi katika mji mkuu wa nchi hiyo, Quito.

Ecuador Präsidentschaftskandidat Fernando Villavicencio wurde in Quito erschossen
Picha: Karen Toro/REUTERS

Taarifa hiyo imetolewa na rais Rais wa Ecuador Guillermo Lasso aliyesema kuwa kitendo hicho hakitofumbiwa macho na kitaadhibiwa vikali. Lasso amesisitiza kuwa, kwa hili  makundi ya uhalifu  yamechupa mipaka na yatakabiliwa na mkono wa sheria.

Ofisi ya mwanasheria mkuu wa Ecuador imesema mshukiwa katika kesi hiyo mauaji ya Villavicencio amefariki dunia kutokana na majeraha aliyoyapata wakati wa kukamatwa kwake.

Polisi wamethibitisha kuwa watu wengine kadhaa wamejeruhiwa, wakiwemo maafisa wake, katika tukio walilosema ni kitendo cha kigaidi na kuahidi kufanya uchunguzi wa kina.

Villavicencio mwenye umri wa miaka 59 na mwenye watoto watano, alikuwa mmoja wa wagombea wanane katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Agosti 20 mwaka huu na alikuwa mwanachama wa Vuguvugu lenye dhamira ya Kuijenga Ecuador.

Fernando Villavicencio akiwa kwenye kampeni ya urais muda mchache kabla ya kuuawa. Quito, Ecuador: 09.08.2023Picha: Karen Toro/REUTERS

Muda mchache kabla ya kuuawa kwa mgombea huyo wa urais nchini Ecuador,  Villavicencio alikuwa ameapa kupambana dhidi ya ufisadi na makundi ya uhalifu:

" Lidumu jiji la Quito ambako tumeacha historia ya mapambano yetu makubwa dhidi ya dhulma. Katika jiji hili tutaacha pia historia ya vita vyetu vya demokrasia katika uchaguzi ujao. Tuaacha historia ya mapambano dhidi ya ufisadi, magenge ya uhalifu yaliyotishia nchi yetu kwa miaka 20. Ndugu zangu, katika uchaguzi wa Agosti 20, itakuwa ni mapambano majambazi na watu wema wanaotaka kuiokoa nchi hii."

Fernando Villavicencio alikuwa pia mkosoaji mkubwa dhidi ya ufisadi hasa wakati wa serikali ya Rais wa zamani Rafael Correa kuanzia mwaka 2007 hadi 2017. Aliwasilisha malalamiko mengi mahakamani dhidi ya vigogo wa serikali ya Correa, ikiwa ni pamoja na rais mwenyewe ambaye ametaja kusikitishwa na mauaji hayo.

Soma pia: Watu watano wameuawa Ecuador

Mauaji hayo yanajiri huku kukiwa na wimbi la ghasia katika taifa hilo la Amerika ya Kusini, linaloshuhudia pia ongezeko la biashara ya dawa za kulevya, mauaji ya kikatili huku watoto wakiajiriwa na magenge ya uhalifu.

Mauaji hayo yalaaniwa na watu mbalimbali

Wafuasi wa Villavicencio wakiwa katika taharuki wakati wa ufyatuaji risasi, 09.08.2023Picha: STRINGER/AFP/Getty Images

Mshauri wa kampeni wa Villavicencio Patricio Zuquilanda amesema mgombea huyo alipokea vitisho vya kuuawa kabla ya tukio hilo, na aliporipoti taarifa hizo kwa mamlaka husika na kuzuliwa kwa siku moja.

Zuquilanda amesema watu wa  Ecuador  wana majonzi na taifa hilo limejeruhiwa vibaya, huku akitoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuchukua hatua dhidi ya ghasia hizo.

Balozi wa Marekani nchini humo Mike FitzPatrick pamoja na wagombea wengine wa urais kama Luisa Gonzalez, Daniel Noboa Azin na Xavier Hervas wamelaani vikali mauaji hayo.

Jumuiya ya nchi za Amerika Kusini imewataka wagombea hao kuimarisha usalama wao na kusema usalama wa wagombea ni msingi wa kudumisha imani katika mfumo wa kidemokrasia.

(RTRE,APE)

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW