1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Edward Lowassa: Mwanasiasa hodari au mwoga?

12 Februari 2024

Hakuwa mwanasiasa wa kawaida kwa hakika. Edward Ngoyai Lowassa ameacha urathi wa kipekee. Wako watakaosema alikuwa shujaa na mtu jasiri. Wengine watamkumbuka kama mwanasiasa mwoga na asiye msimamo.

Tanzania| Edward Lowassa
Lowassa alikuwa mbunge wa Monduli hadi alipogombea urais mwaka 2015.Picha: Getty Images/AFP/T. Karumba

Alikuwa waziri mkuu wa kwanza kujiuzulu kwa kashfa nchini Tanzania. Na kwa miaka mingi baadaye akaandamwa na kivuli cha tuhuma za rushwa na ufisadi.  

Edward Ngoyai Lowasa alizaliwa Agosti 26 mwaka 1953. Baba yake alikuwa mfugaji katika wilaya ya Monduli, huko Arusha kaskazini mwa Tanzania. Yeye alikuwa mtoto wa nne. Safari yake ya siasa ilianza tangu mwishoni mwa miaka 1980. Aliteuliwa mara mbili kuwa waziri kwenye serikali ya rais Ali Hassan Mwinyi.  

Nyota ya Lowasa iling´aa zaidi alipoteuliwa kuwa waziri wa maji na maendeleo ya mifugo baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2000.  

Mtindo wake wa kuchapa kazi uliwavutia wengi. Ufuatiliaji makini wa miradi, kuepuka tabia ya kuwabembeleza watumishi na kuwawajibisha waliokuwa wazembe vilimjengea sifa machoni mwa umma.  

Alifananishwa wakati huo na aliyekuwa waziri mkuu wa zamani wa Tanzania Edward Moringe Sokeine. Alikuwa miongoni mwa mawaziri waliopachikwa jina la "askari wa mwavuli” na rais Benjamin Mkapa. 

Rais wa zamani wa Tanzania, hayati Benjamin Mkapa, kushoto, alimtaja Lowassa, kulia, kuwa mmoja wa "askari wa mwavuli.'Picha: DW/Said Khamis

Waziri Mkuu aliebeba matumaini ya Tanzania mpya

Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005  ulifungua njia kubwa zaidi kwa Lowassa. Jakaya Mrisho Kikwete, mwanasiasa aliyetajwa kuwa sahibu mkubwa wa Lowasa alichaguliwa kura rais wa Tanzania.  

Tetesi kwamba Lowasa angekuwa waziri mkuu wa nane wa taifa hilo zilisadifu kuwa kweli. Jina lake lilipotajwa bungeni mnamo Disemba 29, 2005, lilipokewa kwa shangwe na kuidhinishwa kwa wingi mkubwa wa kura.  

Soma pia: Lowassa asema demokrasia hairudishiki nyuma

Chini ya kauli mbiu ya uchaguzi ya "ari mpya, nguvu mpya, kasi mpya” Lowasa aliingia madarakani akibeba matumaini ya watanzania wengi. Kauli na hatua zake za siku za mwanzo kabisa zilidhihirisha kuwa taifa limepata kiongozi aliye tayari kulifanyia mageuzi. 

Lakini yote hayo hayakudumu muda mrefu. Kiasi miaka miwili baadaye, Lowasa, kiongozi aliyetoa taswira ya matumaini na utumishi ulitukuka akatumbukia shimoni.

Kashfa ya Richmond ilisadifu kuwa kihunzi kirefu kwa Lowasa. Alituhumiwa kutumia nafasi yake kurefusha mkataba wa kampuni hewa ya Richmond iliyopewa kandarasi ya kufua umeme.  

Kamati ya bunge iliyofanya uchunguzi wa kasfha ya Richmond, ilisema Lowasa alipuuza ushauri wa kampuni ya taifa ya kufua umeme, TANESCO na kushinikiza kurefushwa mkataba wa Richmond.  

Uamuzi huo uliligharimu taifa mabilioni ya shilingi. Kamati hiyo iliyoongozwa na mbunge wa jimbo la Kyela, Harrison Mwakyembe ilisema kampuni hewa Richmond ilikuwa ikipokea dola 100,000 za marekani kila siku bila kuzalisha hata wati moja ya umeme.  

Lowaasa alilazimishwa kujiuzulu uwaziri mkuu kufuatia kashfa ya ufisadi iliyotikisa utawala wa rais Jakaya Kikwete mwaka 2008. Picha: DW

Kashfa ya Richmond na anguko la Lowassa

Ilikuwa kashfa iliyolitikisa taifa na utawala wa rais Jakaya Kikwete. Wabunge wa chama tawala na upinzani walitoa michango mikali mikali kwenye ukumbi wa bunge. Ilikuwa dhahiri kuwa waziri mkuu aliyeingia madarakani kwa ahadi ya mageuzi asingeweza kusalimika. Hatimaye Februari 7 2008 Edward Lowasa alisalimu amri.  

Wako wanaoamini kashfa ya Richmond ilikuwa mkakati wa kumwondoa Lowasa madarakani kutokana na makundi ndani ya chama tawala. Inatajwa lengo lilikuwa ni kumzuia kuwania urais mwaka 2015 baada ya Kikwete kumaliza muhula wake. Juu ya iwapo simulizi hiyo ina ukweli hakuna anayeweza kusema.  

Soma pia: Zanzibar: Lowassa na Seif Sharif wazungumzia mkwamo

Mwanasiasa huyo hakuwahi kufikishwa mahakamani wala kupata nafasi rasmi ya kujitetea kuhusu uhusika wake kwenye kashfa ya Richmond.  

Mwenyewe tangu wakati huo hadi kifo chake aliendelea kukanusha kuhusika na kashfa hiyo 

Hilo lakini halikumwondolea mzigo wa lawama. Jina lake liliingia doa ambalo halikufutika kwa miaka mingi. Kila lilipotajwa watu walilihusisha na mwanasiasa asiye mwaminifu, mwizi wa fedha za walipa kodi na aliyelitia hasara taifa.  

Kashfa ya Richmond imebakia kuwa kovu la maisha ya siasa ya Lowasa hadi kifo chake. Huenda hasara kubwa zaidi ilikuwa ni kuparaganyika kwa mahusiano yake na rais Kikwete. Na hilo lilikuja kugharimu ndoto za Lowasa kuwa rais wa Tanzania miaka 8 baadaye. 

Kutafuta mabadiliko nje ya CCM

Mwaka 2015 wakati anamaliza muhula wake wa miaka kumi, kinyang´anyiro cha kumpata mrithi wake kilikuwa kikali ndani ya chama tawala.  

Baada ya jina lake kukatwa CCM, Lowassa alifanya uamuzi uliotikisa siasa za Tanzania kwa kujiunga na chama cha upinzani Chadema, alikogombea urais dhidi ya mgombea wa chama tawala John Pombe Magufuli.Picha: Getty Images/AFP/D. Hayduk

CCM iligawika vipande. Lowasa ambaye alikuwa wakati huo amepigwa chapa ya ufisadi, alifanikiwa kutengeneza kundi lenye nguvu. Kundi la wanasiasa waliomtetea kuwa hakuhusika na kashfa ya Richmond. CCM nusura ipasuke vipande wakati wa mchakato wa kupata mgombea wake mjini Dodoma.  

Licha ya ushawishi mkubwa aliokuwa nao Lowasa, jina lake lilienguliwa katika hatua za mapema na kuzusha kishindo kikubwa. Hatimaye lakini John Pombe Magufuli ndiye aliteuliwa kuwa mgombea wa chama cha mapinduzi.  

Soma pia: Edward Lowassa na safari ya matumaini

Wiki chache baadae chama cha mapinduzi kilipata pigo ambalo hakikutarajia. Kada wake wa miaka mingi na waziri mkuu wa zamani Edward Lowasa alikihama chama hicho. Ulikuwa uamuzi ulitikisa jukwaa la siasa Tanzania. Aliteuliwa kuwania urais kupitia kikuu cha upinzani; CHADEMA, chini ya mwavuli wa vyama vya upinzani uliojulikana kama UKAWA. 

Uamuzi wa Lowasa kuhamia chadema ulifungua njia ya kuufanya uchaguzi wa mwaka 2015 kuwa wa aina yake nchini Tanzania.  

Kama ilivyokuwa mwaka 1995, wnaasiasa wawili  waliolelewa ndani ya chama cha mapinduzi walikuwa wanachuana kuwania kiti cha urais wa Tanzania, John Magufuli  ndani ya chama hicho na

Faida na hasara za Lowassa kuhamia upinzani

This browser does not support the audio element.

Ulikuwa uchaguzi usio mfano, hasa katika wakati ambapo chama cha mapinduzi kilikuwa kinapitia misukosuko mingi ya kashfa za rushwa na ufisadi na utendaji mbaya.   

Zilikuwa kampeni za mapambano makali, CCM wakimnadi Magufuli kuwa mwanasiasa atakayerejesha nidhamu serikali na kumpaka tope Lowasa kuwa mgombea aliyejaa madoa. Upinzani nao ulikuwa ukijibu mapigo.  

Hata hivyo uchaguzi huo ulimalizika kwa John Magufuli kupata ushindi.

Lowassa aamua kurejea nyumbani CCM

Katika kile kilichokuja kudhihirika kuwa uamuzi alioufanya kwa shauku yake ya kuwa rais wa Tanzania, Edward Lowasa alirejea kwenye chama cha mapinduzi miaka minne baada ya uchaguzi wa mwaka 2015.

Soma pia:  Edward Lowassa arejea CCM

Alikutana na rais John Magufuli na kuzika tofauti za wakati wa uchaguzi. 

Hali ya afya ya Edward Lowasa ilikuwa ikijadiliwa sana miaka ya karibuni. Ilimulikwa zaidi wakati wa kampeni za uchaguzi wa mwaka 2015. 

Kwa muda mrefu alionekana dhaifu mwenye kujikokota. Uvumi kuwa anasumbuliwa na maradhi makubwa ulisambaa mara kadhaa. Hata wakati mwingine alizushiwa kifo. 

Baada ya kukaa upinzani kwa miaka michache, Lowassa aliamua kurudi nyumbani CCM mwaka 2019, ambapo alisalia kuwa mwanachama hadi mauti yalipomfika.Picha: DW/S. Khamis

Tangazo la kifo chake mnamo Februari 10 mwaka 2024 lilizusha simanzi kubwa chini Tanzania. Bila ya shaka kifo cha Lowasa kinahitimisha enzi ya mwanasiasa aliyetimiza vyote isipokuwa ndoto ya kuwa rais wa Tanzania.  

Yeyote anayetizama nyuma maisha ya Lowasa anaweza kusema alikuwa mwanasiasa kigogo. Mtu aliyejipambanua kuwa mtumishi mahiri wa umma lakini aliyeshia kuitia doa mwenyewe haiba yake.

Ikiwa tafsiri halisi ya maisha ya mwasiasa ni safari ya kupanda na kushuka basi kwa nchini Tanzania pengine hakuna aliyetimiza hilo maishani kumshinda Edward Ngoyai Lowasa.  

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW