1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Edward Lowassa atapeperusha bendera ya UKAWA

20 Oktoba 2015

Baada ya ndoto yake ya kuiongoza Tanzania kusambaratishwa kupitia kamati ya maadili ya chama tawala - chama cha Mapinduzi CCM, Edward Lowassa anaendelea na safari yake ya matumaini kupitia njia nyingine.

Tansania Wahlen Edward Lowassa
Picha: Getty Images/AFP/D. Hayduk

Waziri mkuu wa zamani Edward Ngoyayi Lowassa alikuw ana uhakika wa kuchukuwa uongozi wa juu wa chama cha mapinduzi, hadi kamati ya maadili ilipofanya uamuzi wake wa mwisho juu ya watangaza nia 38 waliokuwa wanawania nafasi ya kukiwakilisha chama katika uchaguzi wa rais, na kumuengua mapema kwenye kinyanganyiro cha kurithi nafasi ya rais Jakaya Kikwete, bila hata kuingizwa kwenye tano bora.

Akiwa amedhamiria kuendeleza ndoto yake ya kuliongoza taifa hilo kubwa kabisa na lenye wakaazi wengi zaidi Afrika Mashariki, Lowassa alijiondoa kwenye chama tawala, kupinga jinsi mchakato wa kumteua mgombea ulivyoendeshwa - na kuwaqtuhumu viongozi wa juu wa chama kwa kukiuka katiba ya chama na kuminya demokrasia, kwa kutowapa nafasi wanachama kuchagua mgombea wanaemtaka.

"CCM siyo baba yangu na wala siyo mama yangu, "alisema Lowassa wakati akitangaza uamuzi wa kujiondoa kwenye chama hicho alichokitumikia tangu kuanzishwa kwake mwaka 1977, na kuongeza kuwa iwapo wananchi hawawezi kupata madadiliko wanayoyataka kupitia CCM, watayapata nje ya CCM - kauli maarufu iliyotumiwa na rais wa kwanza wa taifa hilo Mwalimu Julius Nyerere katika miaka ya 1990. Lowassa alisema kuendelea kuwepo ndani ya CCM kama itakuwa unafiki.

Lowassa alijondoa CCM baada ya jina lake kukatwa na kamati ya maadili ya chama hicho tawala.Picha: Getty Images/AFP/T. Karumba

Wakati ushindi wa CCM katika chaguzi nyingi zilizopita ulikuwa jambo lisilo na mashaka - wakati ambapo vyama vya upinzani vilikuwa vimeparaganyika na kushindwa kutoa changamoto ya kweli kwa chama hicho, hatua ya Lowassa kuhamia upinzani inaonekana kubadili mwelekeo wa siasa za taifa. Idadi kubwa ya mahudhurio kwenye kampeni za upinzani katika wiki za karibuni, imekuwa kielelezo tosha kwamba kujiunga kwake kumeongeza mhemuko na hamasa katika siasa tepetepe za taifa hilo.

Lowasa ni nani?

Edward Ngoyayi Lowassa alizaliwa Agosti 26, 1953 katika wilaya ya Monduli, mkoani Arusha, ambako alianzia elimu yake ya msingi katika shule ya msingi ya Monduli mwaka 1960. Baadaye alijiunga na shule ya sekondari ya Arusha kati ya mwaka 1967 na 1971 kwa kidato cha kwanza hadi cha nne, na kisha aliendelea na masomo ya juu katika shule ya Sekondari ya Milambo (sasa St. Mary's) ya mjini Tabora mwaka 1973.

Mwaka 1974, Lowassa alijiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa masomo ya shahada yake ya kwanza ya Sanaa na Elimu, na kuhitimu mwaka 1977, kabla ya kusafiri kwenda nchini Uingereza mwaka 1983 ambako alijiunga na chuo kikuu cha Hull kwa shahada ya uzamili ya sayansi ya maendeleo ya jamii.

Safari yake ya kisiasa

Akiwa katika chuo kikuu cha Dar es Salaam, Lowassa alianza kushiriki siasa kwa kujiunga na kisha kuwa kiongozi wa tawi la vijana wa chama Tanganyika African National Union (TANU). Ni mwanasiasa nguli na mzoefu nchini Tanzania, akiwa ameshikilia nyadhifa kadhaa, ikiwemo ya uwaziri mkuu kati ya mwaka 2005 na 2008, alipolaazimishwa kujiuzulu kwa kuhushwa na sakata la kampuni bandia ya kufua umeme ya Richmond.

Alipotangaza uamuzi wake wa kujiondoa CCM na kujiunga na Chadema.Picha: DW

Lowassa amekanusha mara zote kuhusiana na kampuni hiyo na hivi karibuni alieleza kuwa akiwa waziri mkuu alikuwa ameamua kuvunja mkataba wa kampuni hiyo lakini uamuzi wake ulivinjwa na kile alichokitaja kuwa maagizo kutoka juu. Chama chake kipya cha Chadema kimekuwa kikidai tangu wakati huo kuwa mhusika mkuu wa Richmond ni rais Jakaya Kikwete, kutokana na maelezo hayo ya Lowassa.

Kama ilivyo kwa mpinzani wake katika kinyanganyiro hicho, Lowassa pia anajulikana kuwa mtendaji maahiri na wanaothubutu kuchukuwa maamuzi magumu. Kati ya mwaka 2000 hadi 2005, akiwa waziri wa maji na maendeleo ya mifugo, alichukuwa uamuzi wa kuvunja mkataba wa kampuni ya City Water aliopewa jukumu la kutoa huduma za maji kwa wakaazi wa Dar es Salaam na maeneo jirani, baada ya kampuni hiyo kushindwa kutekeleza wajibu wake ipasavyo.

Baadhi ya mafanikio yake ni pamoja na mchango wake katika kufanikisha utandazaji wa bomba la kusambaza maji kutoka ziwa Victoria kwenda mikoa ya Mwanza na Shinyanga, bila kusahau juhudi zake za kurekebisha mfumo wa upimaji viwanja uliyosaidiwa kupunguza kero za umiliki wa ardhi alipokuwa waziri wa ardhi, nyumba na maendeleo ya makaazi kati ya mwaka 1993 na 1995.

Ahadi zake kwa wapiga kura

Ameahidi kushughulikia changamoto kuu zinazoikabili Tanzania, likiwemo suala la elimu, ambayo bado inashindwa kutoa wahitimu wenye ushindani na hata baadhi kushindwa kuipata kutokana na gharama kubwa, akiahidi kutumia mapato yatokanayo na rasilimali za taifa hilo kufanikisha azma hiyo.

"Mwenyezi Mungu ametujaalia gesi asilia. Ninaamini fedha zinazotokana na gesi yetu zinapaswa kuelekezwa katika kuboresha sekta ya elimu ...., wazazi wengi hawamudu kulipia gharama za elimu kwa watoto wao. Ikiwa tutatumia fedha hizo tunaweza kuwasaidia watoto wao kupata elimu bora. Ndiyo maana nasisitiza kwamba tunahitaji kuelekeza nguvu kwenye elimu na kilimo baadae, kwa sababu mtu mwenye elimu bora atafanya vizuri kwenye kilimo," anasema.

Lowassa akiwahutubia wafuasi wa upinzania katika moja ya kampeni zake za kuwania urais.Picha: Getty Images/AFP/D. Hayduk

Lowassa anaamini umaskini unaweza tu kuondolewa kupitia mfumo shirikishi - ambao unawawezesha watu wa kipato cha chini kutambua changamoto zinazowakabili, na kutambua njia bora za kushughulikia changamoto hizo. "Kuwashirikisha raia kunawawezesha kupanga shughuli zao za kimaendeleo, kujiwekea malengo na kushiriki njia za kuyafanikisha," ananukuliwa na wavuti ya kampeni yake ya teamlowassa2015.com

Wakosoaji wake hata hivyo wanasema tamaa ya madaraka isiyo kifani ndiyo ilimsukuma Lowassa kujiondoa kwenye chama chake na kujiunga na upinzani.

Tangu alipojitoa CCM na kuhamia Chadema, chama tawala kimeondokewa na baadhi ya vigogo wake wake wakiwemo waziri mkuu mwingine wa zamani Fredrick Sumaye, Mzee Kingunge Ngombale Mwiru - moja wa makada waanzilishi wa CCM na hivi karibuni, katibu mkuu wa zamani wa Jumuiya ya Afika Mashariki Balozi Juma Mwapachu, ambao wote ni marafiki wa karibu wa Lowassa.

CCM hata hivyo inasisitiza kwamba kujiondoa kwa makada wake na wengine waliomfuata Lowassa Chadema hakutishii madaraka yake iliyoyahodhi kwa miaka 54 sasa. Lakini wakati ambapo hata Lowassa amedhamiria kutimiza ndoto yake ya muda mrefu - na ishara zikionyesha hii ndiyo nafasi ya mwisho aliobakiza kutimiza ndoto hiyo - wangalizi wanasema uchaguzi wa mwaka huu utatoa changamoto kubw azaidi kwa chama cha CCM, ambacho ni moja ya vyama vichache vya uhuru vinavyoendelea kushika madaraka barani Afrika.

Mwandishi: Iddi Ssessanga

Mhariri: Saumu Yusuf