1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Eid El Fitr yenye simanzi nchini Iraq

Tuma Provian Dandi12 Oktoba 2007

Hali ya amani imeendelea kuwa mbaya nchini Iraq baada ya Majeshi ya Marekani kufanya mashambulizi yaliiyouwa watu 15 wakiwa wanawake na watoto.

Ndege za kijeshi za majeshi ya Washirika nchini Iraq
Ndege za kijeshi za majeshi ya Washirika nchini IraqPicha: AP

Wakati Sherehe ya Eid El Fitr ikianza, wananchi wa Iraq wamekumbwa na simanzi kubwa baada ya majeshi ya Marekani kufanya shambulizi lililoua watu 15 wakiwa ni wanawake na watoto.

Hilo ni tukio kubwa na la aina yake lililogharimu maisha ya watu wema katika kipindi hiki cha shamshara shamra baada ya mfungo Mtukufu wa Ramadhani.

Pamoja na vifo hivyo vya wanawake na watoto vilivyotokea katika eneo la Ziwa Tharthar Kaskazini Magharibi mwa mji wa Baghdad, pia majeshi ya Marekani yamekiri kufanya mauaji dhidi ya wapiganaji 19.

Jeshi la Marekani limejitetea kwa kukiri kwamba vifo hivyo vya wanawake na watoto 15 vimetokea kwa bahati mbaya wakati wakijaribu kuangamiza kikundi cha wanaharati waliokuwa katika maeneo yenye raia hao.

Taarifa zaidi imeeleza kwamba majeshi ya marekani yaliwaona wanaharakati hao walioelezewa kwamba ni wanachama wa mtandao wa Al Qaeda na wafuasi wa Rais wa zamani Bwana Saddam Hussein, waliokuwa wakikutana karibu na ziwa Tharther.

Aidha, katika eneo la Tuz kilometa 200 Kaskazini mwa Baghdad, mtu mmoja wa kujitoa muhanga amefanya shambulizi jingine lililouwa mwanaume mmoja na mtoto wake baada ya kulipua bomu lililokuwa limetegwa katika mkokoteni. Watu wengine 20 wamejuruhiwa kwenye eneo hilo walipokuwa wakisherehekea sikukuu ya Eid El Fitr.

Msemaji wa polisi wa eneo hilo Hiwa Abdullah, amesema mwanaume huyo alijaribu kukwepa mlipuko wa bomu hilo lakini alikuwa tayari amechelewa, hivyo kupoteza maisha yake na ya mwanae.

Hata hivyo polisi wamesema mtu huyo aliyepanga kujitoa muhanga hakuuawa na kwamba hali yake ni mbaya baada ya kukatika mguu mmoja na kupata majeraha mengine makubwa.

Huenda vifo zaidi vikatokea katika shamrashamra hizi za sikukuu ya Eid zilizoanza kwa waumini wa madhehebu ya Sunni nchi Iraq, kwa kuwa wengi wao wanazitumia kwenda kwenye mikusanyiko mbalimbali ikiwemo kuwatembelea ndugu, jamaa na marafiki.

Wakati vifo hivi vipya vikitokea, hapo jana mtu mwingine wa kujitoa muhanga alielekeza gari lake lenye mabomu katika mgahawa mmoja wa internet uliokuwa na vijana wengi na kufanikiwa kuuwa watu wanane papo hapo na kujeruhi wengine 25 mjini Baghdad.

Uchunguzi unaonesha kwamba vifo vya leo vya wanawake na watoto siyo vya kwanza kufanywa na majeshi ya Marekani dhidi ya raia wema nchini Iraq, na muda wote mauaji kama hayo yanapotokea, majeshi hayo yamekuwa yikijitetea kwamba wapiganaji walijichanganya na raia.

Tukio jingine la kusikitisha lilitokea mwanzoni mwa mwezi uliopita, ambapo pia majeshi ya washirika yaliwauwa raia 15 na kisha kuomba radhi kwa madai kwamba shabaha yao haikuwa sahihi.

Kwa mujibu wa tovuti ya Iraq, karibu raia wema elfu 81 wameshauawa tangu kuanza kwa vita ya iraq mwaka 2003.