Ekpo: mwanasiasa wa kwanza wa kike Nigeria
Margaret Ekpo aliishi wapi na wakati gani? Margaret Ekpo alizaliwa mwaka 1924 katika mji wa Creek katika jimbo la Cross River, Kusini Mashariki mwa Nigeria. Wakati huo, Nigeria ilitawaliwa na Uingereza na wanawake hawakuruhusiwa kupiga kura. Ekpo aliaga dunia akiwa na umri wa miaka 92 mwaka 2006, Calabar katika jimbo la Cross River.
Ni nini kinachokumbukwa kuhusu Margaret Ekpo? Ekpo anakumbukwa hususan kwa kuwaleta pamoja wanawake masikini na matajiri kupigania haki zao za kiuchumi na kisiasa na kushiriki katika uchaguzi. Aidha alijitolea bila kuchoka kutetea uhuru wa taifa la Nigeria. Alikuwa mmoja wa wanasiasa wa kike wa kwanza aliyechaguliwa na akaendelea kupigania nafasi ya mwanamke alipokuwa mwanasiasa.
Margaret Ekpo alijitosa vipi kwenye siasa? Katika miaka ya 1940, Ekpo ambaye mumewe alikuwa daktari, alianza kuhudhuria mikutano ya maandamano ya kupinga jinsi wafanyakazi wa huduma za hospitali Nigeria walivyokuwa wakiangaliwa na mamlaka ya ukoloni wa Uingereza.
Mwaka 1946, alianzisha Chama cha Wanawake Sokoni, ili kuwaweka katika mshikamano wanawake katika mji wa Aba kwenye jimbo la Abia ambako alikuwa akiishi na mumewe.
Katika kipindi hicho, Ekpo pia alijishughulisha katika harakati za Nigeria za kuupinga ukoloni. Alijiunga na Chama cha Baraza la Kitaifa la Nigeria na Cameroon. Chama hicho kilimteua kuwa mwanachama maalum kwenye Bunge la jimbo lenye ushawishi kuwakilisha wanawake.
Baada ya Nigeria kupata uhuru kutoka Uingereza mwaka 1960, Ekpo alichaguliwa kisiasa kuwa mbunge wa mkoa wa Mashariki. Alikuwa mwanamke wa kwanza eneo la Aba na mmoja wa wanawake wachache nchini kuchaguliwa katika wadhifa kama huo.
Kwenye mahojiana na DW; Etubong Essien mwenzake Ekpo, alisema Margaret aliwajibika moja kwa moja kwa wanawake wengi waliokuwa wanajitosa kwenye siasa.
"Alikuwa mtendaji, mzungumzaji mzuri pia. Wakati huo, wanawake wengi hawakushiriki kwenye siasa lakini aliwahimiza. Waliingia kwenye siasa na wakapewa nafasi hasa wale waliofanikiwa kuchaguliwa kuingia bungeni."
Kama mwanasiasa, Ekpo aliendelea kupigania hali bora ya kiuchumi na kisiasa kwa wanawake, kwa mfano alishinikiza kuboreshwa kwa barabara zilizokuwa zinaelekea masokoni.
Nini kilichofanyika baadaye? Ekpo alikuwa mwanasiasa aliyechaguliwa hadi vita vya wenyewe kwa wenyewe vilipoanza mwaka 1967. Wakati wa vita hivyo, alizuiliwa na mamlaka ya Biafra kwa miaka mitatu, wakati mmoja akawa mgonjwa sana kwa kukosa chakula cha kutosha. Mwaka 2001, Rais wa Nigeria wakati huo Olusegun Obasanjo, alibadilisha jina la uwanja wa ndege wa Calabar karibu na mji alikozaliwa na kuupa jina lake. Kwa sasa unaitwa Uwanja wa Kimataifa wa Ekpo. Hatua hiyo ni kumbukumbu ya mchango wake Ekpo kwa ustawi wa taifa lake.
Pinado Abdu-Waba na Gwendolin Hilse wamechangia katika makala hii. Ni sehemu ya makala maalum za mfululizo wa "Asili ya Afrika", ushirikiano kati ya shirika la DW na taasisi ya Gerda Henkel.
Mwandishi: Pinado Abdu-Waba na Gwendolin Hilse
Tafsiri: Shisia Wasilwa
Mhariri: Saumu Yusuf