El-Sissi: Mazungumzo ya kusitisha vita Gaza yanatia moyo
8 Oktoba 2025
Rais wa Misri Abdel-Fattah el-Sissi ametuma ujumbe rasmi kwa Rais wa Marekani Donald Trump akimkaribisha katika mji wa Bahari ya Shamu wa Sharm el-Sheikh, ambako kunafanyika mazungumzo hayo kati ya ujumbe wa Hamas na Israel.
el-Sissi ametoa ujumbe huo kupitia hotuba iliyopeperushwa na televisheni ya taifa akimkaribisha Rais Trump, kuhudhuria hafla ya kutiwa saini kwa makubaliano ya kusitisha mapigano katika Ukanda wa Gaza, iwapo makubaliano hayo yatafikiwa.
"Ujumbe wangu kwa Rais Trump, namwambia hivi: Mheshimiwa rais, endelea na juhudi zako za kuvimaliza vita hivi. Ninashukuru kwa kila kitu unachokifanya katika eneo hili, na itakuwa jambo jema ikiwa makubaliano yatafikiwa ukiwepo. Nakualika Trump, Mungu akipenda kuhudhuria hafla ya utiaji saini wa makubaliano hayo nchini Misri."
Mazungumzo hayo ya kusitisha mapigano yameingia siku yake ya tatu hii leo yakihusisha maafisa wa ngazi kutoka Marekani, Israel na nchi zinazosaidia juhudi za upatanishi – ishara ya dhamira ya kweli kwamba wajumbe hao wanakusudia kushughulikia masuala yoyote nyeti yatakayoibuka kuhusu mpango wa Marekani wa kuvimaliza vita katika ukanda wa Gaza.
Erdogan aisifu Hamas kwa kukubali mpango wa amani
Hamas imeweka wazi kwamba inataka dhamana kutoka kwa Rais Donald Trump na nchi wadhamini kwamba Israel haitaendelea tena na operesheni zake za kijeshi Gaza mara baada ya kundi hilo la wanamgambo kuwaachilia huru mateka wote waliobaki - wanaokadiriwa kuwa 20.
Kwa upande wake, Rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan amelisifu kundi la Hamas kwa kuukumbatia mpango wa amani wa Rais Trump huku akielezea Israel kama "kizuizi kikubwa zaidi” kwa amani.
Akihutubia wabunge wa chama chake tawala, kiongozi huyo amesema amani haiwezi kupatikana kwa kuiwekea Hamas na Wapalestina jukumu lote, na kwamba kufanya hivyo sio sahihi, na wala sio haki.
Ameyataja mazungumzo yanayoendelea mjini Sharm al-Sheikh, kuwa "muhimu sana” na akaonyesha matumaini kuwa yatazaa matunda.
"Usitishaji wa mapigano na amani ya haki ni chaguo lenye mantiki zaidi kwa pande zote. Mazungumzo yaliyofanyika leo huko Sharm el-Sheikh yana umuhimu mkubwa. Tunatumai tutapokea habari njema."
Wakati huo huo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Marco Rubio, anatarajiwa kuhudhuria mkutano wa mawaziri utakaofanyika kesho Alhamisi mjini Paris pamoja na viongozi wengine kutoka mataifa ya Ulaya na Kiarabu.
Kwa mujibu wa vyanzo vya kidiplomasia, mkutano huo, ambao utafanyika sambamba na mazungumzo yanayoendelea nchini Misri, unalenga kujadili jinsi ya kutekeleza mpango wa Trump na kutathmini ahadi za pamoja za nchi husika kuhusu Gaza.
Huko Gaza kwenyewe, Wapalestina wengi wamepoteza makaazi yao huku wakikabiliwa na njaa na ukosefu wa huduma za msingi ikiwemo mafuta, maji, na vifaa vya matibabu.
Wizara ya Afya ya Gaza inayosimamiwa na Hamas imesema mashambulizi ya Israel yamewaua watu wanane katika eneo hilo katika muda wa saa 24 zilizopita - idadi ndogo zaidi ya vifo kuripotiwa katika kipindi cha wiki moja iliyopita.