Ellen Johnson Sirleaf ashinda uchaguzi Liberia
11 Novemba 2011Tume ya uchaguzi nchini humo hapo jana ilitangaza kuwa kutokana na matokeo yaliyokusanywa kutoka asilimia 86.6 ya vituo vya upigaji kura Sirleaf alishinda uchaguzi huo kwa asilimia 90.8, huku naye Tubman akijikusanyia asilimia 9.
Ni asilimia 37.4 ya watu milioni 1.8 nchini humo waliopiga kura huku wengi wakiaminika kuwa walisalia nyumbani kutokana na wito huo wa kuususia uchaguzi na kuzuka kwa vurugu mkesha wa kuamkia siku yenyewe ya uchaguzi, wakati polisi ilipambana na waandamanaji wa upinzani.
Ujumbe wa Carter wa waangalizi 52 umesema kuwa uchaguzi huo ulifanyika kwa uwazi, licha ya kuwa, uchaguzi huo ulisusiwa na upinzani, kukumbwa na vurugu hizo na kuwepo idadi ndogo ya wapiga kura, jambo ambalo lmeelezwa kuwa ni la kusikitisha.
Marekani imetoa wito kwa raia nchini humo kukubali kwa amani matokeo hayo.
Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Marekani, Mark Toner, aliwaambia waandishi habari kuwa Marekani ina wasiwasi na imeelezea wasiwasi wake kuhusu vurugu zilizozuka kabla ya uchaguzi huo na kuwa inaendelea kutazama matukio kwa makini nchini humo.
Sirleaf ambaye ni rais wa kwanza mwanamke barani Afrika, anakabiliwa na awamu ya pili iliyo ngumu huku taifa lake likiwa limezidi kugawanyika baada ya uchaguzi huo kuingia dosari. Hapo jana rais Sirleaf alieleza kuwa uchunguzi kamili utafanyika kuhusu vurugu hizo za Jumatatu.
Amevinyoshea mkono wa urafiki vyama vya upinzani akisema kuwa anatumai kuunda serikali inayojumuisha pande zote kama alivyofanya wakati aliposhinda uchaguzi wa mwaka 2005 miaka miwili baada ya kumalizika kwa mzozo wa miaka 14 nchini humo.
Waangalizi wameeleza kuwa rais huyo mpya atakabiliwa na changamoto za uhalali wa uongozi wake, ambapo amechaguliwa kwa mara nyengine katika uchaguzi ambao upinzani haukushiriki, lakini hili rais Sirleaf amelipinga.
Uchaguzi huo unaonekana kama nafasi ya nchi hiyo iliyokumbwa na vita vya kiraia, kuimarisha demokrasia yake dhaifu, na kuimarisha amani, miaka minane baada ya kumalizika mzozo huo uliosababisha vifo vya kiasi ya watu laki mbili na nusu.
Wakati matokeo ya kwanza yalipotangazwa kwenye radio nchini humo, wananchi barabarani walionekana wakisherehekea. Kiongozi wa chama kikuu cha upinzani, Congress for Democratic Change, CDC, Winston Tubman, ambaye zamani alikuwa afisa wa Umoja wa mataifa, amesema hatoyatambua matokeo ya awamu hiyo ya pili ya uchaguzi, kutokana na kile alichosema kuwa makosa yaliyodhihirika katika awamu ya kwanza.
Rais Sirleaf amesema wakati awamu yake ya kwanza ililenga kuimarisha amani na maendeleo, hii ya pili ataitumia kukabiliana na matatizo kama vile ukosefu wa ajira, unaozidi kukithiri kwa asilimia 80 nchini humo.
Mwandishi: Maryam Abdalla/Dpae/Afpe
Mhariri:Josephat Charo