1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
JamiiMarekani

Mmiliki wa Twitter Elon Musk atangaza kuachia ngazi

21 Desemba 2022

Mmiliki wa Twitter Elon Musk hatimaye amesema ataachia uongozi wa kampuni hiyo maarufu ya mitandaoni, mara tu atakapopata mtu wa kurithi kiti cha Mkurugenzi Mkuu.

Elon Musk Umfrage auf Twitter
Picha: Yui Mok/PA Wire/picture alliance

Baada ya kukaa kimya kwa muda mrefu na kisha kutoa kauli za kukanganya juu ya kura ya maoni ya mtandaoni aliyoiitisha mwenyewe, mmiliki wa  Twitter Elon Musk hatimaye amesema ataachia uongozi wa kampuni hiyo maarufu ya mitandaoni, mara tu atakapopata mtu wa kurithi kiti cha Mkurugenzi Mkuu.

Baada ya wiki kadhaa za mvutano na kuahirishwa kuhusu mustakabali wa mtandao huo wa kijamii tangu alipoinunua Twitter kwa euro bilioni 44, Elon Musk aliwauliza watumiaji ikiwa anapaswa kuondoka au la kwa ukuu wa jukwaa hilo.

Haikuwa mara ya kwanza kwa mmiliki huyo bilionea kutumia njia hiyo ya maoni, kwani tayari alikwishaitumia mara kadhaa, ikiwa ni pamoja na kurejesha akaunti ya rais wa zamani wa Marekani Donald Trump, pamoja na watumiaji wengine waliosimamishwa.

Kila wakati, Musk alipoahidi kuheshimu matokeo ya utafiti ambao aliuanzisha, mara nyingi matokeo yalikwenda katika mwelekeo aliotarajia.

Asilimia 57 ya watumiaji wa Twitter wanataka Musk aondoke katika uongozi

Matajiri Elon Musk und Jared Kushner wakiandala sokaPicha: Dan Mullan/Getty Images

Lakini wakati huu, 57% ya watumiaji takriban milioni 17 wa jukwaa hilo waliopiga kura walisema wanaunga mkono kuondoka kwake.

Baada ya kuwasili Marekani Jumatatu kutoka Doha alikokwenda kutazama fainali za Kombe la Dunia, Elon Musk alisalia kwanza kimya, kabla ya kujibu kupitia  Twitter akidokeza kuwa matokeo ya kura hiyo ya maoni yalitokana na njama za makusudi pamoja na watumiaji bandia kupotosha mtazamo halisi wa watumiaji.

Siku ya Jumanne, mmiliki huyo wa Twitter alichapisha matokeo aliyodai yalikusanywa na kwa kutumia sampuli binafsi za watumiaji wa Twitter, ambayo yalionyesha kuwa asilimia 61 walitaka Elon Musk aendelee kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Twitter.

''Kwa hali ya kushangaza inaelekea tunalo tatizo kubwa watumiaji bandia,'' alisema mmiliki huyo wa Twitter, katika kilichochukuliwa kama azma ya kung'ang'ania uongozini.

Halafu alitangaza kuwa kura yoyote nyingine ya maoni kupitia jukwaa lake, itapigwa tu na watumiaji wanaolipia huduma hiyo.

Soma zaidi:Twitter yairejesha akaunti ya Trump

Pale vyombo kadhaa vya habari vya nchini Marekani viliporipoti kuwa hata kabla ya kutangaza kura yake ya maoni mtandaoni, Elon Musk alikuwa tayari akimtafuta Mkurugenzi Mtendaji mpya, tajiri huyo alijibu tu kwa kejeli kwa emoji.

Hata hivyo, matokeo hayo ya kura ya maoni mtandaoni na hata uvumi uliofuatia havionyeshi kumdhuru Elon Musk. Kinyume chake, thamani ya kampuni ya magari ya Tesla anayoimiliki ilipanda kwenye soko la mitaji, licha ya ukosoaji unaoongezeka dhidi ya Musk kwamba hivi sasa anaijali sana Twitter kuliko kampuni hiyo.