1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Emir wa Qatar azuru Kigali na Kinshasa

21 Novemba 2025

Kiongozi wa Qatar SheikhTamim bin Hamad Al-Thani amekamilisha ziara rasmi ya siku mbili nchini Rwanda na kuelekea mjini Kinshasa ambako anatazamiwa kukutana kwa mazungumzo na Rais Felix Tshisisekedi.

Marekani | Tamim bin Hamad Al Thani akihutubia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mjini New York Septemba 20, 2022
Emir wa Qatar Sheikh Tamim bin Hamad Al Thani akizungumza katika kikao cha 77 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA) katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa mnamo Septemba 20, 2022 jijini New York.Picha: Anna Moneymaker/Getty Images

Akiwa mjini Kigali, Rwanda Sheikh Tamim bin Hamad Al-Thani alifanya mazungumzo ya faragha na Rais wa Rwanda Paul Kagame, ingawa haikuelezwa wazi kiini cha mazungumzo yao.

Ziara ya kiongozi wa Qatar imekuja wakati ambapo mzozo wa mashariki mwa Kongo ukizidi kuimarika kutokana na utata wake. Qatar ni mpatanishi wa serikali ya Kinshasa na waasi wa kundi la AFC/M23 ambao hadi sasa wanaendelea kupambana na serikali huku wakiyakamata maeneo mengi mashariki mwa nchi hiyo kubwa zaidi katika ukanda wa maziwa makuu. Hata hivyo mkataba baina yao na serikali uliosainiwa mjini Doha wiki iliyopita hadi sasa haujasaidia kusitisha mapigano.

Kwa upande mwingine Marekani ambayo ni mshirika wa karibu na Qatar inaendelea kuwa mpatanishi kati ya Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia Kongo.

Ziara hii ya Emir wa Qatar mjini Kigali na Kinshasa inafanyika katika sura mbili za kiuchumi na kiusalama katika jitihada za kuimarisha usalama wa miradi yake katika eneo la Maziwa Makuu.

Kiuchumi, Qatar kwa muda mrefu imekuwa mshirika wa karibu wa Rwanda hasa katika miradi mikubwa ya uwekezaji katika usafiri na usafirishaji wa anga, utalii pamoja na usalama. Mapema mwaka huu nchi mbili zilitia saini mkataba wa kuwaondolea visa wananchi kutoka nchi moja kwenda nyingine.

​​​​Ndege za shirika la ndege la Qatar, ambayo inamiliki asilimia 60 ya uwanja wa ndege wa kimataifa unaojengwa Kigali, RwandaPicha: Jan Woitas/dpa/picture alliance

Kwa upande wa uwekezaji wa kiuchumi pia serikali ya Qatar inamiliki asilimia 60 za uwekezaji katika uwanja mpya wa  kimataifa wa ndege unaoendelea kujengwa mashariki mwa mji mkuu wa Rwanda Kigali huku ndege za shirika la ndege Qatar zikifanya safari mjini Kigali mara 4 kwa wiki.

Baadhi ya wadadisi wa kiuchumi na kisiasa wanahisi ziara ya kiongozi huyu wa Qatar imeua ndege wawili kwa jiwe moja kwa kuzingatia maslahi yake ya kiuchumi na kiusalama katika eneo la maziwa makuu.

"Ziara kama hii zinakuwa na umuhimu mkubwa katika nyanja za kisiasa, kiuchumi na kidiplomasia, lakini hii pia inaandika historia nyingine katika ushirikiano kati ya Kigali na Doha, lakini pia kiusalama. Ni ziara ambayo imekuja kwa wakati muafaka kutokana na nafasi ya Qatar katika usuluhishi wa mzozo wa mashariki mwa Kongo baina ya serikali ya Kongo na kundi la M23."

Mazungumzo ya kirafiki kati ya marais wa Rwanda na DR Congo Machi 18 huko QatarPicha: AFP

Suala la mkutano baina ya marais wa Rwanda Paul Kagame na mwenzie wa Congo Felix Tshisisekedi hadi sasa limesalia njia panda chini ya usuluhishi wa Marekani. Marais hao awali walipaswa kukutana mjini Washington ili kutia saini mkataba wa kumaliza tofauti zao lakini hadi sasa bado hawajakutana.

Kulingana na uchambuzi wa James Munyaneza mwandishi wa habari mkongwe mjini Kigali na aliyefuatilia mzozo huu wa mashariki mwa Congo kwa muda mrefu anasema ana imani kuwa  sasa ziara ya kiongozi huyo huenda ikabadili ukurasa mzima

Amesema "Naamini kwamba ziara ya Emir wa Qatar itawezesha kuwepo kwa mazingira mazuri na rahisi kwa hawa marais wawili hatimaye kukutana iwe mjini Washington au maeneo mengine ili hatimaye wapate suluhisho la kisiasa na la kuleta amani kumaliza mzozo huo."

Nchi za Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ambazo ni wadau wakubwa wa Qatar  kutokana na uwekezaji ambao nchi hiyo ndogo ya kiarabu imeuwekeza katika mataifa hayo mawili jirani lakini yenye uadui wa paka na panya.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW