1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Emmanuel Macron ndiye kiongozi mpya wa Ulaya?

Oumilkheir Hamidou
9 Januari 2018

Kansela Angela Merkel wa Ujerumani alikuwa amezowea kuwa kiongozi mwenye ushawishi zaidi barani Ulaya. Hivi sasa rais wa Ufaransa Emmanuel Macron anaonekana kuanza kumpiku taratibu: Lakini kila mmoja anamhitaji mwenzake.

Angela Merkel und Emmanuel Macron
Picha: imago/Reporters

Kwa miaka sasa Angela Merkel  ndie aliyekuwa na kauli ya mwisho katika Umoja wa Ulaya na hilo hakuna aliyekuwa akilibisha. Baada ya ushindi wa Donald Trump nchini Marekani, wengi na hasa  mongoni mwa wahariri wa magazeti yanayozungumza Kiiegereza waliashiria Angela Merkel "angekuwa kiongozi wa dunia huria.

"Hali hiyo iliendelea kuwa hivyo hadi miezi michache iliyopita.Tangu uchaguzi mkuu ulipoitishwa Septemba mwaka jana nchini Ujerumani, Angela Merkel  na chama chake cha CDU  sio tu  wamepoteza kura, bali pia  Merkel amesalia kuwa kiongozi wa mpito na mpaka sasa bado hajafanikiwa kuunda serikali mpya.

Rais Macron akitoa hotuba ya mwaka mpya kwa waandishi wa habari katika Kasri la Elysee, Januari 3,2018.Picha: picture alliance/AP Photo/L. Marin

Kwa upande wa pili  Emmanuel Macron anaonyesha kuibuka kuwa nyota mpya inayong'ara katika anga la kisiasa barani Ulaya. Macron, kijana mwenye haiba ameng'ara kwa kuibuka na ushindi mkubwa uchaguzi wa rais ulipoitishwa nchini Ufaransa dhidi ya kiongozi wa chama cha siasa kali za mrengo wa kulia Marine le Pen. Baadae akafanikiwa pia kuanzisha mageuzi katika sekta ya ajira licha ya upinzani mkubwa uliokuwepo.

Na sasa hali bora ya kiuchumi imeanza kuchomoza. Idadi ya wanaomuunga mkono imeanza kupanda. Katika sherehe za kukamilisha miaka 40, mwezi uliopita wa Decemba, Wafaransa wengi walimtaja Macron "kuwa rais mzuri".

Katika wakati ambapo upande wa upinzani unamtuhumu kutaka kujigeuza "mfalme Napoleon", Macron aliwaahidi Wafaransa katika kampeni zake za uchaguzi atairejeshea hadhi yake nchi yao pindi akishinda.

Nchi nzima ambayo kwa miaka kadhaa sasa haikuwa ikijiamini, inaaonyesha kugutuka na kuanza upya kujiamini tangu  Emmanuel Macron alipoingia madarakani.

Kiongozi anaejiamini katika jukwaa la kimataifa

Na hata katika majukwaa ya kimataifa Emmanuel Macron anajiamini. Ameshawakaribisha rais Donald Trump wa Marekani, na kula naye chakula cha usiku katika mnara wa Eifel, sawa na alivyomkaribisha rais Vladimir Putin wa Urusi katika kasri la Versailles.

Amemudu ipasavyo mkutano wa kimataifa kuhusu mabadiliko ya tabianchi mjini Paris, sera mpya kuelekea Afrika, na pia kumkaribisha rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdggan.

Rais Macron akimkaribisha Rais Racep Tayyip Erdogan wa Uturuki katika kasri la rais la Elysee mjini Paris, Januari 5, 2018.Picha: picture alliance/abaca/Somer

"Anairejeshea Ufaransa hadhi yake ya jadi  katika nyanja za kidiplomasia, anaifanya Ufaransa iwajibike zaidi na kukadiria yanayotokea ulimwenguni yanaihusu pia Ufaransa na Ufaransa inabidi iwajibike," anasema Stefan Seidendorf, naibu mkurugenzi wa taasisi ya uhusiano kati ya Ujerumani na ufaransa mjini Ludwigburg.

Anaongeza kusema Emmanuel Macron anakiri kwamba siasa yake ya nje itapata nguvu tu itakapotambulikana kama siasa ya nje ya Umoja wa Ulaya.

Hata hivyo baadhi ya wakati Macron anacheza karata yake bila ya kumjali mshirika wake Angela Merkel, mfano alipokutana hivi karibuni na rais wa Uturuki mjini Paris. Mtindo wa Macron katika kukabiliana na washirika tete, mfano wa Erdogan na Putin pia ni tofauti na ule wa Angela Merkel.

Mwandishi:Christoph Hasselbach/Hamidou Oummilkheir

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman