Eneo kubwa kabisa dunia la biashara huru kuanzishwa.
17 Novemba 2007Benita Ferrero-Waldner, kamishna wa umoja wa Ulaya anayehusika na uhusiano na mataifa ya nje, amesherehekea mapema mwezi huu hatua zilizopigwa katika mazungumzo juu ya kufungua milango ya biashara baina ya mataifa ya umoja wa Ulaya na washirika wake katika eneo la bahari ya Mediterranean. Iwapo mazungumzo haya yatafanikiwa , amedokeza, eneo huru la biashara litakalohusisha jumla ya watu milioni 740 litaanzishwa.
Lengo hili , ambalo umoja wa Ulaya unamatumaini ya kufikia ifikapo mwaka 2010, limekuwa katika meza ya majadiliano tangu mkutano wa mwaka 1995, kati ya viongozi wa umoja wa Ulaya na wale wa mataifa yanayopakana na bahari ya Mediterranean. Utaratibu wa utendaji katika majadiliano ulijadiliwa hivi karibuni katika mkutano wa mawaziri ambao umoja wa Ulaya ulifanya pamoja na viongozi 12 wa serikali za eneo hilo, Algeria, Misr, Israel, Tunisia, Uturuki, Albania na Mauritania.
Akihutubia mkutano huo , Ferrero-Waldner amedokeza kuwa majadiliano yataendelea kuhusiana na kufungua milango ya biashara katika huduma, pamoja na mazao ya kilimo na uvuvi.
Pamoja na hayo hali ya mafanikio ambayo ameionyesha inakanushwa na uchunguzi uliogharamiwa na taasisi yake, halmashauri ya Ulaya , imeeleza kuwa eneo la biashara huria linaweza kuathiri zaidi hali mbaya iliyopo ya mataifa mengi katika eneo la kusini na mashariki ya bahari ya Mediterranean , ambako zaidi ya asilimia 30 ya watu wanaishi kwa chini ya dola moja kwa siku.
Uchunguzi huo uliofanywa na taasisi ya sera za maendeleo na utawala katika chuo kikuu cha Manchster, umeonyesha kuwa mapato yatakayotokana na kodi katika uagizaji yatapungua kwa kiasi kikubwa mara biashara itakapo kuwa huru, na athari zitaonekana zaidi nchini Lebanon na maeneo ya Palestina.
Kupungua kwa fedha zinazoingia katika hazina za mataifa hayo kutakuwa sawa na asilimia 5 ya pato jumla la taifa GDP, nchini Lebanon na zaidi ya asilimia 2 nchini Tunisia na Morocco. Asasi zisizokuwa za kiserikali zinadai kuwa ugunduzi huo wa utafiti unapuuziwa na viongozi wa umoja wa Ulaya.
Athari za muda mfupi na muda mrefu katika makubaliano ya biashara huria katika Mediterranean yatakuwa kinyume na matarajio, amesema Kinda Mohamedieh kutoka asasi ya Kiarabu ya mfumo wa maendeleo katika mji mkuu wa Lebanon ,Beirut. Anashaka kuwa dhamira halisi ya umoja wa Ulaya katika kusukuma makubaliano hayo ya biashara huria ni kuhakikisha kuwa makampuni ya mataifa ya magharibi yanapata udhibiti wa rasilmali za mataifa hayo.
Miongoni mwa matatizo yanayoweza kusababishwa na kufungua milango ya biashara huru ambayo chuo kikuu cha Manchester kimeyafichua ni pamoja na ongezeko kubwa kabisa la ukosefu wa kazi, kupungua kwa kiwango cha mishahara, shinikizo kubwa katika mazingira kwa upande wa maeneo ya mijini yanayotokana na uhamiaji mkubwa wa watu kutoka vijijini, na hali isiyokuwa salama ya watu masikini kutokana na kubadilika kila wakati kwa bei za bidhaa muhimu za chakula duniani.