1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Pembe ya Afrika ipo hatarini kufuatia uhaba wa mvua

24 Februari 2023

Shirika la kikanda la ufuatiliaji wa masuala ya hali ya hewa limeonya Jumatano kwamba ukame wa kutisha katika Pembe ya Afrika unaoonyesha kila dalili za kuendelea kutokana na ukosefu wa mvua kwa msimu wa sita mfululizo.

Kenia Dürre an der Grenze zu Äthiopien
Picha: Thomas Mukoya/REUTERS

Mamlaka ya Kikanda ya Utabiri wa Masuala ya Hali ya Hewa (ICPAC) imebaini kuwa utabiri wa msimu wa mvua kuanzia mwezi Machi hadi Mei mwaka 2023 unaonyesha kushuka kwa kiwango cha mvua na kuongezeka kwa hali ya joto.

Msimu huu muhimu wa kuanzia Machi hadi Mei kwa kawaida huchangia hadi asilimia 60 ya jumla ya mvua zinazonyesha kwa mwaka katika maeneo mapana ya Ikweta yanayopatikana katika Pembe ya Afrika.

Utabiri huu unathibitisha hofu ya wataalamu na mashirika yanayohusika na masuala ya hali ya hewa, ambao wamekuwa wakionya juu ya janga kubwa la kibinadamu ambalo halijawahi kushuhudiwa  wakati ambapo ukame uliodumu kwa muda mrefu na mbaya zaidi ukiendelea kulikumba eneo hilo.

ICPAC yenye makao yake Nairobi ndiyo kituo cha hali ya hewa cha kikanda kilichoteuliwa na Shirika la Hali ya Hewa Duniani, na katika taarifa yake imesema kuwa katika sehemu za Ethiopia, Kenya, Somalia, na Uganda ambazo zimeathiriwa zaidi na ukame wa hivi karibuni, huu unaweza kuwa msimu wa sita mfululizo wa ukosefu wa mvua.

Soma pia:Ukame wayaweka maisha ya mtoto wa kike hatarini, Kenya 

Mbuga ya Kitaifa ya Tsavo nchini Kenya inayokabiliwa na ukame: Septemba 30, 2022. Huku ukame ukiendelea kuathiri mifugo na watu huko Afrika Mashariki, wanyamapori nchini Kenya wanakufa nchini humo. Picha: Andrew Wasike/AA/picture alliance

Pembe ya Afrika ni moja wapo ya maeneo yaliyo hatarini zaidi kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa, na matukio mabaya ya hali ya hewa yamekuwa yakishuhudiwa kila mara na kwa viwango vya kutisha.

Misimu mitano mfululizo ya uhaba wa mvua imesababisha vifo vya mamilioni ya mifugo, kuharibu mazao, na kuwalazimisha zaidi ya watu milioni moja kuyahama makazi yao ili kutafuta maji na chakula.  

Kulingana na Shirika la Maendeleo la eneo la Afrika Mashariki na Pembe ya Afrika, IGAD pamoja na shirika la Umoja wa Mataifa la Kilimo na Chakula, FAO, ICPAC imesema hali katika siku zijazo ni mbaya zaidi kuliko nyakati za ukame wa mwaka 2011, huku watu milioni 23 katika nchi za Kenya, Ethiopia na Somalia wakiwa tayari wanakabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula.

Njaa kuongezeka kutokana na ukame

Kenya inapambana na ukame na uhaba wa chakula, Eldama Ravine, Kenya (03.09.2022)Picha: DW

Kulingana na Umoja wa Mataifa, mwaka huo hali ya njaa ilitangazwa nchini Somalia, na baadhi ya watu 260,000 huku nusu ya watu hao wakiwa ni watoto wenye umri chini ya miaka sita, walikufa kwa njaa, na miongoni mwa sababu ikiwa ni kukosekana kwa hatua za haraka za jumuiya ya kimataifa. Wakati huo, eneo hilo lilikuwa na misimu miwili duni ya mvua.

 

Mada inayohusiana: 

Madhara ya ukame huko Kitengela, Kajiado nchini Kenya

04:28

This browser does not support the video element.

 

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema siku ya Jumatano kuwa watu milioni 1.3, huku asilimia 80 kati yao wakiwa ni wanawake na watoto, wamelazimika kuyahama makazi yao nchini Somalia kutokana na ukame unaoendelea.

Licha ya kuwa viwango vya juu vya njaa havikufikiwa, Guterres amesema watu milioni 8.3 ikiwa ni zaidi ya nusu ya wakazi wa Somalia watahitaji msaada wa kibinadamu mwaka huu.

Workneh Gebeyehu, katibu mtendaji wa IGAD, ametoa wito wa kuongezwa kwa haraka hatua za kupunguza hali ya hatari katika Pembe ya Afrika, huku akizitaka mamlaka za kitaifa, watendaji wa masuala ya kibinadamu na maendeleo kuchukua hatua mbadala kabla hali haijawa mbaya zaidi.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW