1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Migogoro

Tigray iko hatarini kukabiliwa na mgogoro mpya

23 Februari 2026

Hali ya wasiwasi yaongezeka Tigray, wakati vita vikinukia kati ya jeshi la serikali kuu, wanamgambo wa Tigray na jeshi la Eritrea huku wakaazi wa huko wakijikuta kwa mara nyengine katikati ya mkwamo wa maisha usiokwisha.

Äthiopien Hawzen 2021 | TPLF-Kämpfer an Wachposten
Picha: Ben Curtis/AP/picture alliance

Gebreegziabher Berehe ameacha kuwangojea watalii kuwasili kwani wengi wanahofia kuanza tena upya. Muongoza wageni huyo wa Tigray anasema idadi ya watalii wanaotaka huduma yake imeshuka, mashine za kutolea pesa mjini Mekele, mji mkuu wa mkoa huo, ni tupu, naye anafikiria kuihama nchi ambayo hawezi tena kumudu maisha yake.

Berehe mwenye umri wa miaka 37 anasema ikiwa vita vitarudi tena, vitakuwa vibaya zaidi kuliko vya mwanzo, na kwamba yeye na wenzake sasa wanakabiliwa sio tu na hali mbaya ya maisha bali pia ya kimaadili, hata kabla ya kusikia mlio wowote wa risasi. Mjini Mekele kwenyewe kuna ukimya wa ajabu, lakini wasiwasi umeongezeka baina ya mamlaka za mkoa huo na serikali kuu ya Ethiopia mjini Addis Ababa.

Makubaliano ya amani ya Novemba 2022 yaliyokomesha vita vilivyouwa maelfu ya watu wakati jeshi la Ethiopia likiungwa mkono na Eritrea lilipopambana na wanamgambo wa huko, saa yako hatarini kuvunjika.

Serikali ya mkoa wa Tigray inazituhumu mamlaka za Addis Ababa kwa kuyavunja makubaliano hayo kwa kufanya mashambulizi ya droni. Wakati huo huo, serikali ya Ethiopia inaituhumu Eritrea kwa kuyaandaa na kuyalipa makundi yenye silaha ndani ya Tigray, inayopakana nayo.

Wadadisi: Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed, anasisitiza ulazima wa nchi yake kuwa na fursa ya kutumia Bahari ya Shamu na hilo huenda likachochea mgogoro zaidiPicha: Office of the Prime Minister-Ethiopia

Kauli za Abiy Ahmed huenda zikachochea vita

Kinachoweza kutokea sasa, ni marafiki wa zamani kubadilishana pande za vita: Eritrea inaweza kushirikiana na mahasimu wao wa zamani, Jeshi la Ukombozi wa Watu wa Tigray, TPLF, ambalo ndilo linaloitawala Tigray, dhidi ya vikosi vya Ethiopia, ambavyo kwenye vita vilivyopita walikuwa ndio washirika wao.

Vita vilivyomalizika mwaka 2022 vilikuwa vibaya sana, vikiwa na matukio mengi ya dhuluma za kingono na kuwanyima watu chakula kama silaha ya kivita.

Wakaazi wengi wa Mekele wanazinga njia ya kukimbia mapigano mapya muda huu wanapoweza kufanya hivyo, wakikumbuka mambo yalivyokuwa kwenye vita vilivyopita, ambapo mawasiiano yalikatwa na serikali ya Ethiopia ikaweka marufuku ya kusafiri mkoa mzima.

Wadadisi wa mambo wanasema huenda vita vya mara hii vinachochewa na Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed, ambaye anasisitiza ulazima wa nchi yake kuwa na fursa ya kutumia Bahari ya Shamu, ambayo kimsingi iko Eritrea. Kabla ya kujitwalia uhuru wake mwaka 1993, Eritrea ilikuwa sehemu ya Ethiopia baada ya miongo kadhaa ya vita vya msituni.

Abiy aliwaambia wabunge mapema mwezi huu kwamba Bahari ya Shamu na Ethiopia haziwezi kuendelea kutenganishwa daima, kauli ambayo ilikosolewa vikali na serikali ya Eritrea iliyosema ni ndoto ya hatari.

Picha: Alexander Joe/AFP/dpa/picture-alliance

Eritrea yahofia bandari yake kushambuliwa kijeshi

Eritrea ikihofia mashambulizi ya kijeshi dhidi ya bandari yake ya Assab imejibu kwa kuwachangamsha mahasimu wao wa zamani, viongozi wa Tigray, hata kama inakanusha kuwa na ushirika wowote.

Hilo limezusha wasiwasi mjini Addis Ababa, ambako serikali ya Ethiopia imewaita wanajeshi wake wa akiba. Tangu alipoingia madarakani mwaka 2018, Abiy amekuwa akijaribu kuijengea nchi taswira ya taifa linaloinuka kiuchumi, kijeshi na kisiasa, lakini amekuwa akirejeshwa nyuma na migogoro mbalimbali kwa miaka kadhaa sasa.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, amezitaka pande zote kujizuwia, kauli inayosadifiana na ile ya Umoja wa Ulaya na Uingereza, ambazo zote zimewaonya raia wao kutokwenda kwenda kwenye mkoa huo.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW