1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

England imeiondoa Ujerumani "Euro 2020"

30 Juni 2021

Mjini London nchini Uingereza ulikuwa usiku mgumu kwa Ujerumani baada ya England kuifungisha virago maarufu kama "Die Mannschaft" baada ya kuichapa mabao 2-0.

EURO 2020 | Deutschland vs England
Picha: Catherine Ivill/REUTERS

Ushindi wa England katika mchuano huo unatajwa kuifikisha mwisho umwamba wa Ujerumani dhidi ya timu yao uliodumu kwa takribani miaka 55.

Ilikuwa dakika 75 katika kipindi cha pili pale ambapo winga machachari wa timu ya Manchester City, Raheem Starling alipolichungulia lango la Ujerumani,  hatua ambayo ilitekelezwa pia na Harry Kane katika dakika ya 86,  aliyewainua mashabiki 45,000 wa soka wa England katika uwanja wa Wembley.

England yavunja rekodi kwa kuifunga Ujerumani.

Watu maarufu wa England wakiutazama mchuanoPicha: Carl Recine/REUTERS

Rekodi zinaonesha ni ushindi wa kwanza kwa Uingereza dhidi ya Ujerumani katika mashindano makubwa kama haya ya euro 2020, tangu mwaka 1966, katika mchuano uliopigwa katika uwanja wa zamani wa Wembley ambapo Ujerumani ilichapwa mabao 4-2.

Uingereza ambayo kwa sasa imeingia katika hatua ya robo fainali, Jumamosi ijayo itashuka dimbani mjini Roma kwa mara nyingine kufuana na Ukraine ambayo iliibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Sweden. Na baadae, endapo itaibuka na ushindi katika mchuano huo itarejea mjini London kwa michezo yote itakayosalia.

Mashaka ya hatma ya  kocha wa  wa Ujerumani Joachim Loew baada ya kichapo.

Kocha wa timu ya Ujerumani Joachim Loew.Picha: John Sibley/REUTERS

Hatua ya kutolewa Ujerumani katika mchuano huo inaweza kuwa ndio mwisho mbaya kwa kocha wake Joachim Loew, ambae amedumu katika kukinoa kikosi hicho cha taifa kwa takribani miaka 15. Kocha huyo nyota yake iliwaka katika mnyukano wa kombe la dunia la 2014.

Tukijikita kidogo katika mchuano mwingine ambao ulitupiwa jicho sana na mashabiki wa soka wa Ukraine na Sweden. Kama ilivyodokezwa hapo awali Sweden nayo imebanduliwa katika hatua hiyo ya mtoano kwa kupigwa mabao 2-1 na Ukraine. Ushindi wa Ukraine ulipatakina katika muda wa ziada katika kipute hicho kilichopigwa katika uwanja wa Glasgow.

Baada ya ushindi huo, kocha wa Ukraine  Andriy Shevchenko amejitamba kwamba hawatishwi na England pamoja na kwamba timu hiyo imeipiga Ujerumani.