1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MichezoUfaransa

Enrique awataka wachezaji wake kuwa makini zaidi

29 Aprili 2026

Kocha wa PSG Luis Enrique amesema timu yake italazimika kucheza kwa umakini mkubwa na kufunga mabao zaidi ugenini dhidi ya Bayern Munich wiki ijayo ili kuhakikisha inafuzu fainali nyingine ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Ligi ya Mabingwa barani Ulaya - Fainali - Paris St Germain v Inter Milan
Kocha wa Paris Saint‑Germain Luis EnriquePicha: Kai Pfaffenbach/REUTERS

Kauli hiyo ameitoa baada ya miamba hao wa Ufaransa Paris Saint‑Germain kupata ushindi wa mabao 5–4 katika mchezo wa kwanza wa nusu fainali uliochezwa jijini Paris.

Enrique ambaye aliiongoza PSG kutwaa taji hilo msimu uliopita, amekiri kuwa matokeo hayo hayatoshi kuwapa uhakika wa kufuzu.

Kocha huyo ameeleza kuwa mazingira ya ugenini Allianz Arena yanahitaji kiwango cha juu cha umakini na ubunifu wa kushambulia. Amesisitiza kuwa ili kuwa salama, PSG inapaswa kufunga angalau mabao matatu katika mchezo wa marudiano dhidi ya Bayern Munich.

Mchezo huo wa kwanza umeingia kwenye historia kama nusu fainali yenye mabao mengi zaidi katika enzi ya sasa ya Ligi ya Mabingwa, ukionyesha ubora wa safu za ushambuliaji za timu zote mbili pamoja na changamoto katika safu zao za ulinzi. Mashabiki na wachambuzi wa soka wameutaja mchezo huo kuwa moja wa mechi za nusu fainali zenye ushindani mkubwa na kusisimia kuwahi kutokea.

Mshindi wa pambano hilo atatinga fainali itakayofanyika mjini Budapest, ambako atakutana na mshindi kati ya Arsenal na Atletico Madrid. Timu hizo mbili zinamenyana leo usiku katika nusu fainali ya pili, huku kila upande ukitafuta nafasi ya kuingia kwenye fainali ya mashindano hayo makubwa barani Ulaya.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW