Erdogan aahidi hatua kali dhidi ya "wasaliti"
16 Julai 2017Akizungumza mbele ya umati wa watu waliohudhuria kumbukumbu za mwaka mmoja za jaribio hilo jana Jumamosi (15 Julai) katika daraja mjini Istanbul, Erdogan alisema: "Wale wasaliti watakumbukwa daima kwa kuchukiwa," akiongeza kwamba Uturuki "haijawahi kusita kuvunjavunja vichwa vya wale wanaosaliti."
Pia ameahidi "kuwakata vichwa wasaliti kwanza," akimaanisha magaidi, katika hotuba ambayo iliambatana na rejea za maandiko ya Kiislamu na ukosoaji mkubwa dhidi ya upinzani.
Erdogan aliongeza kwamba wafungwa waliokamatwa kwa kuhusika na jaribio la mapinduzi sasa wanavaa "sare zinazofanana na Guantanamo mahakamani, akimaanisha gereza lenye utata la Marekani nchini Cuba.
Hotuba hiyo katika daraja la Bosporus, ambalo lilipewa jina jipya la daraja la mashahidi mwaka jana na lilikuwa moja ya sehemu za mapaigano katika jaribio la mapinduzi mwaka 2016, yaliyofanyika mbele ya maelfu ya watu waliokuwa wakipepea bendera ya Uturuki.
Erdogan pia alishiriki katika maadhimisho ya usiku wa manane mjini Ankara kwa wale waliofariki katika jaribio hilo la mapinduzi, wakati wabunge wa upinzani walisusia tukio hilo.
Upinzani waishutumu serikali
Hapo mapema siku ya Jumamosi katika mji mkuu, kiongozi wa chama kikuu cha upinzani nchini Uturuki alishutumu kushindwa kwa serikali kuzuwia jaribio la mwaka jana la mapinduzi na hali inayoendelea ya kukamatwa kwa wale wanaodaiwa kuunga mkono mapinduzi wakati wa kikao maalum cha bunge kuadhimisha mwaka mmoja tangu kusjhindwa kwa jaribio hilo la mapinduzi.
Kemal Kilicdaroglu, kiongozi wa chama cha siasa za wastani za mrengo wa kushoto cha People's Republican Party (CHP) aliwashutumu viongozi wa serikali kwa kudai kwamba maafisa ambao waliruhusu waliokula njama ya mapinduzi "kujipenyeza katika maeneo nyeti ya serikali" wawajibishwe.
Serikali inamlaumu imamu anayeishi uhamishoni nchini Marekani, Fethullah Gulen, kwa kuhusika na jaribio hilo la mapinduzi la Julai 15, ambaye aliwahi kuwa mshirika mkubwa wa chama tawala cha Justice and Development (AKP).
Wafuasi wa Gulen walidaiwa kuweza kujipenyeza katika utaratibu wa utawala na jeshi na kufanya jaribio hilo lililoshindwa, lakini Gulen amekana kuhusika na jaribio hilo.
Maswali mengi yanaendelea kubaki juu ya jaribio hilo, ikiwa ni pamoja na kutambua nani hasa anahusika na lini serikali ilifahamu njama hizo. Baadhi ya maafisa wa jeshi wanaoshutumiwa kuwa ni wapangaji wa jaribio hilo wanakana kuwa na mahusiano na Gulen.
Serikali imeitangaza tarehe 15 Julai kuwa sikukuu ya kitaifa ya "demokrasia na umoja" kwa kulieleza jaribio lililoshindwa kuwa ni ushindi wa kihistoria kwa demokrasia nchini Uturuki.
Mwandishi: Sekione Kitojo/afpe/dpae
Mhariri: Mohammed Khelef