1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Erdogan aapa kutotetereshwa na vitisho vya Marekani

11 Agosti 2018

Rais Recep Tayyip Erdogan ameapa kutotii vitisho vya Marekani kuhusiana na mchungaji anaezuwiliwa nchini Uturuki, huku mzozo baina ya washirika hao wa NATO ukizidi, na kusababisha kuporomoka sarafu ya Uturuki la Lira.

Türkei | Erdogan
Picha: picture-alliance/dpa/AP/B. Ozbilici

Rais huyo wa Uturuki alisema pia kuwa ushirika wa nchi yake na Marekani unaweza kuwa katika hatari, akionya kuwa Ankara huenda ikaanza kutafuta washirika wapya, katika makala ya maoni alioiandika katika gazeti la New York Times.

Uhusiano kati ya washirika hao wakubwa wa NATO umeshuka kwa kiwango cha chini kabisaa katika ipindi cha miongo kadhaa, kuhusiana na mkururu wa masuala, yakiwemo kuzuwiliwa kwa mchungaji wa Kimarekani Andrew Brunson kwa tuhuma za ugaidi, na kupelekea thamani ya sarafu ya Uturuki ya Lira kuporomoka dhidi ya dola.

Sarafu ya Lira ilishuka kwa asilimia 16 dhidi ya dola siku ya Ijumaa, na kushuka zaidi baada ya rais wa Marekani Donald Trump kusema ameongeza maradufu viwango vya kodi vinavyotozwa kwenye bidhaa za chuma na bati kutoka Uturuki.

"Ni makosa kuthubutu kuifanya Uturuki isalimu kuptia vitisho kuhusiana na mchungaji," alisema Erdogan katika mji wa bahari nyeusi wa Unye. "Hamna haya, hamna haya," alisema katika matamshi yake yalioelekezwa moja kwa moja kwa serikali mjini Washington. Mnabadilishana mshirika wenu wa kimkakati kwa mchungaji."

Trump alitangaza viwango hivyo vya adhabu kupitia mtandao wa Twitter, akisema "Uhusiano wetu na Uturuki siyo mzuri kwa wakati huu!" Ikulu ya White House imesema vikwazo vipya vilivyowekwa vitaanza kutekelezwa Agosti 13.

Waziri wa fedha wa Uturuki, Berat Albayrak akihutubia mkutano wa waandishi habari kuhusu ruwaza mpya ya uchumi wa nchi katika kasri la Dolmabahce mjini Istanbul, Agosti 10,2018.Picha: picture-alliance/M. Alkac

Wana dola, sisi tunaye Allah

Lakini Erdogan amepuuza mgogoro wa sarafu, na kuwashauri Waturuki kuonyesha mshikamano kwa kubadilisha dhahabu walizoweka au fedha zozote za kigeni kwa Lira ya Uturuki katika juhudi za kushinda kile alichokiita vita vya uhuru dhidi ya Marekani. "Kama wanazo dola, sisi tunaye Allah," alisema.

Na pia alipuuzilia mbali kodi mpya.

"Wanasema hatutoa hiki au kile. Msitoe. Tulivyo navyo vinatutosha."    

     

Katika gazeti la New York Times, Erdogan aliionya Washington kutohatarisha uhusiano wake na Ankara, akisema itatafuta "marafiki wapya na washirika."

Hadi Marekani itakapoanza kuheshimu  mamlaya ya Uturuki na kuonyesha kwamba inafahamu hatari linazokabiliana nazo taifa letu, ushirika wetu unaweza kuwa hatarini," aliandika.

"Kabla haijachelewa, Washington inapaswa kuachana na mawazo pototfu kwamba uhusiano wetu unaweza kuwa wa namna isiyo pacha na kukubaliana na ukweli kwamba Uturuki ina njia mbadala," alisema.

Kushindwa kubadili mwelekeo huu wa maamuzi ya upande mmoja na kutoheshimiana kutatulaazimu kuanza kutafuta marafiki wapya na washirika."

Waziri wa mambo ya nje wa Iran Mohammed Javad Zarif alijitosa pia katika mzozo huo unaozidi makali, na kuituhumu Washington kwa kile alichokiita uraibu wa vikwazo na uonevu." Furaha ya Trump katika kumsababishia madhila ya kiuchumi mshirika wa NATO Uturuki ni aibu," aliandika Zarif kwenye ukurasa wa Twitter.

Mwanaume akiangalia viwango vya ubadilishanaji fedha nje ya duka mjini Istanbul, Ijumaa Agosti 10, 2018. Sarafu ya Lira iliporomoka thamani yake baada ya Rais wa Marekani Donald Trump kutangaza viwango vipya vya kodi kwenye bidhaa za Uturuki.Picha: picture-alliance/AP Photo/M. Yapici

"Marekani inapaswa kurekebisha uraibu wake kwa vikwazo (na) uonevu, vinginevyo dunia nzima itaungana -- zaidi ya ukosoaji wa maneno -- kuilaazimisha kufanya hivyo. Tumesimama na majirani zetu hapo kabla, na tutafanya hivyo tena leo," alionya.

Iran yajitosa upande wa Uturuki

Iran pia ilikumbwa na kuporomoka kwa sarafu yake mwaka huu kwa sehemu kutokana na kurejeshwa kwa vikwazo vya Marekani baada ya Trump kuutupilia mbali mkataba wa nyuklia uliofikiwa mwaka 2015.

Erdogana alifanya mazungumzo kwa njia ya simu na Rais wa Urusi Vladmir Putin siku ya Ijumaa kujadili masuala ya kiuchumi na kibiashara na pia mgogoro wa Syria.

Mzozo huu wa kribuni kati ya Ankara na Washington, umelaaniwa na vyombo vya habari vya Uturuki, ambapo gazeti la kila siku linaloegemea serikali la Sabah lilisema "Shambulizi la sarafu" halikuwa tofauti na jaribio la mapinduzi la Julai 2016.

Kukamatwa kwa mchungaji kumezidi kuvuruga uhusiano na Washington, ambao tayari ulikuwa mashakani. Lakini rais Erdogan aliapa hakutakuwa na kulegeza sheria katika kesi ya Brunson, akisema: hatujatoa tahfifu kwenye sheria mpaka sasa, na kamwe hatutatoa hata moja."

Trump ameelezea kuzuwiliwa kwa mchungaji kama "fedheha kubwa" na kumtaka Erdogan kumuachia "mara moja."

Mwandishi: Iddi Ssessanga/afpe.

Mhariri: Yussra Buwayhid

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW