Erdogan aelekea Saudi Arabia
28 Aprili 2022Rais Recep Erdogan wa Uturuki leo alhamisi anakwenda Saudi Arabia katika ziara yake ya kwanza tangu mwaka 2017, ikiwa ni hatua kubwa ya kurudisha mahusiano baina ya nchi hizo mbili kufuatia mvutano uliokuweko uliotokana na mauaji ya mwandishi habari wa Kisaudi katika ubalozi mdogo wa nchi hiyo mjini Istanbul.
Ziara hii ya rais Erdogan nchini Saudia ndiyo ya hivi karibuni kabisa ya juhudi za Uturuki kujenga tena mahusiano na mahasimu zake wa kikanda.Kwenye ziara hiyo ya siku mbili rais Erdogan anakuwa na mazungumzo na maafisa wa Saudi Arabia katika mji wa pwani ya bahari ya Sharm wa Jiddah na mazungumzo hayo yatajikita hasa kuhusu njia za kuimarisha uhusiano baina ya mataifa hayo mawili kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na ofisi ya rais huyo wa Uturuki.
Pande zote mbili zitabadilishana mawazo kuhusu masuala ya kikanda na kimataifa. Lakini pia maafisa wa Saudi Arabia wameeleza kwamba ziara hiyo itatuwama kwenye masuala ya kurudisha uhusiano wa kawaida baina ya nchi hizo na kurudisha ushirikiano uliokuwepo huko nyuma.
Ni ziara ya kwanza ya rais Erdogan katika taifa hilo la kifalme kuwahi kuifanya tangu mwaka 2017,mwaka mmoja kabla ya kuuliwa Jamal Khashoggi. Aliwahi wakati mmoja rais Erdogan kusema bila ya kumtaja jina mwanamfalme Mohammed bin Salman,kwamba amri ya kuuliwa Khashoggi ilitoka ngazi za juu za Saudi Arabia.
Na itakumbukwa kwamba mwezi uliopita Uturuki ilifuta kesi dhidi ya Wasaudi 26 waliokuwa wakituhumiwa kuhusika na mauaji ya mwandishi habari huyo wa gazeti la WashingtonPost la Marekani, aliyekuwa mkosoaji mkubwa sana wa mrithi wa kiti cha ufalme wa Saudi Arabia,Mohammed bin Salman.
Na hatua hiyo ya Uturuki ilionekana kwa kiasi kikubwa kama namna ya kumfungulia njia rais Erdogan kufanya ziara hii ya kuelekea Saudi Arabia ambako anatarajiwa kukutana na mfalme Salman na mwanawe Mohammed bin Salman.
Na mazungumzo yao pia yatajadili kuhusu migogoro kuanzia wa Yemen,Libya mpaka Syria na kuonesha uungaji mkono kwa Wapalestina.
Katika kipindi cha mwaka mmoja serikali ya mjini Ankara imekuwa mbioni katika juhudi za kidiplomasia kujaribu kutia msukumo wa kurekebisha mahusiano yake na nchi kama Misri,Umoja wa Falme za Kiarabu na Saudi Arabia baada ya miaka ya uhasama uliokuja baada ya vuguvugu la harakati zilizoshuhudiwa katika nchi nyingi za kiarabu mnamo mwaka 2011.
Aidha suala la uthabiti nchini Iraq na mpango wa Nyuklia wa Iran pia yatakuwa kwenye ajenda. Ama baada ya mikutano hiyo rais Erdogan anatarajiwa kwenda Mecca,katika eneo takatifu kushiriki swala za usiku wa mwisho wa mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhan.
Mwandishi:Saumu Mwasimba
Mhariri:Iddi Ssessanga