1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Erdogan aizuru UAE kwa nia ya kuimarisha uhusiano

14 Februari 2022

Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan yupo Umoja wa Falme za Kiarabu UAE kwa mara ya kwanza ndani ya takriban muongo mmoja, ziara inayonuiwa kufufua mahusiano yaliyoyumba kwa muda mrefu kufuatia mivutano ya kikanda.

VAE | Besuch türkischer Präsident Recep Tayyip Erdogan
Picha: Jon Gambrell/AP Photo/picture alliance

Rais Erdogan aliwasili Abu Dhabi katika ziara yake ya siku mbili na kupokewa na Mwanamfalme Sheikh Mohammed bin Zayed Al-Nahyan. Erdogan alikaribishwa pia kwa gwaridel la heshima katika ikulu ya Al-Watan.

Kabla ya kuondoka Istanbul, Erdogan alisema ziara yake imetokana na ziara ya Al Nahyan aliyoifanya mwezi Novemba mwaka jana nchini Uturuki iliyofungua mwanzo mpya wa uhusiano kati ya mataifa hayo mawili. Rais huyo wa Uturuki amesema wamepanga kuchukua hatua zitakazorejesha uhusiano wao mahali unapostahili akiongeza kuwa ushirikiano wa mataifa hayo mawili ni muhimu kwa ajili ya amani na uthabiti wa kanda zima.

Erdogan anatarajiwa kujadili na kusaini  makubaliano 12 ya ushirikiano na UAE kuanzia masuala ya habari na mawasialiano, uchumi, ulinzi, mabadiliko ya tabia nchi, maji na hata usalama wa chakula hii ikiwa ni kwa mujibu wa vyombo vya habari vya Uturuki.

Ziara ya Erdogan imekuja wakati UAE ikikabiliwa na kitisho kinachoongezeka kutoka kwa waasi wa Houthi walioko Yemen wanaoungwa mkono na Iran, waliotekeleza mashambulizi kadhaa kwa kutumia ndege zisizokuwa na rubani pamoja na makombora nchini humo hatua iliyoisababishia UAE kushirikiana kiulinzi na Marekani na Ufaransa.

Mivutano yapungua baada ya Al Nahyan kuizuru Ankara

Mwanamfalme wa UAE Sheikh Mohammed bin Zayed al Nahyan na Rais wa Uturuki Tayyip ErdoganPicha: Turkish Presidency/Murat Cetinmuhurdar/AA/picture alliance

Uturuki na UAE taifa lililo tajiri kwa mafuta zinaunga mkono pande tofauti katika vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Libya na katika migogoro ya Ghuba ya Arabuni. Mataifa hayo mawili yamekuwa yakivutana kwenye masuala mengi hasa suala la gesi mashariki mwa eneo la Mediterrania.

Lakini mivutano hiyo ilipoa moto baada ya mwanamfalme Mohammed bin Zayed, kiongozi wa UAE, kusafiri kuelekea Ankara mwezi Novemba ziara ya kwanza ya kiongozi wa ngazi ya juu tangu mwaka 2012. Alipokuwa huko alitoa dola bilioni 10 za uwekezaji katika taifa hilo ambalo uchumi wake unayumba.

Uhusiano wa Uturuki na Umoja wa falme za kiarabu uliingia doa baada ya Saudi Arabia, Emirati na Bahrain mwaka 2017 kukata mahusiano yao yote na Qatar ambaye ni mshirika wa karibu wa Uturuki.  Mahusiano hayo yalifufuliwa tena mwezi Januari mwaka 2021.

Kuanzia mwaka uliopita, Erdogan amekuwa akijaribu kuimarisha uhusiano wake na maadui zake wa kikanda kutokana na maeneo hayo kutengwa na kusababisha uwekezaji wa kigeni kupungua hasa kutoka nchi za Magharibi.

Mwezi uliyopita alisema ataitembelea Saudi Arabia ikiwa ni ziara ya kwanza tangu uhusiano wao pia kuvunjika kutokana na mauaji ya mwaka 2018 ya muandishi habari, Jamal Khashoggi, aliyekuwa mkosoaji wa serikali ya Saudia na utawala wa Mohammed Bin Salman. Mauaji hayo yalitokea katika ubalozi mdogo wa Uturuki mjini Riyadh.

Chanzo: AFP

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW