Erdogan aondoa pingamizi kwa Sweden kujiunga na NATO
11 Julai 2023Hayo yameelezwa jana usiku na Katibu mkuu wa NATO Jens Stoltenberg ambaye alikutana kwa mazungumzo na Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan na Waziri Mkuu wa Sweden Ulf Kristersson huko Vilnus, Lithuania kunakoanza hii leo mkutano wa kilele wa siku mbili wa NATO.
Hata hivyo, taarifa ya pamoja iliyotolewa na viongozi hao watatu haijabaini ni kwa muda gani Bunge la Uturuki linalazimika kuidhinisha ombi hilo la Sweden.
Stoltenberg amesema kukamilisha ombi la Sweden ni hatua ya kihistoria inayonufaisha usalama wa washirika wote wa NATO hasa katika wakati huu muhimu.
Soma pia: Erdogan aweka sharti jipya kwa Sweden kujiunga na NATO
Biden kukutana na Zelensky huko Vilnius
Rais wa Marekani Joe Biden atakutana hapo kesho kwa mazungumzo na Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy katika mji mkuu wa Lithuania, ambako viongozi wa NATO wamekusanyika katika mkutano wa kilele ambao utatawaliwa na ajenda ya vita nchini Ukraine pamoja na shinikizo la Kyiv la kutaka ikaribishwe haraka ndani ya jumuiya hiyo.
Nchi wanachama wa NATO wanajadili jinsi ya kuondokana na mgawanyiko kuhusu jitihada za Ukraine kuelekea uanachama lakini wanadiplomasia wengi wamebaini kuwa tofauti hizo zimepungua baada ya walio wengi kuafiki kuwa Ukraine haiwezi kujiunga na NATO wakati huu wa vita.
Soma pia:Ukraine:Tumerejesha maeneo yaliodhibitiwa na Urusi
Wanachama wa NATO katika Ulaya Mashariki wameunga mkono msimamo wa Kyiv, wakibaini kwamba, kuijumuisha Ukraine chini ya mwamvuli wa usalama wa pamoja wa NATO ndio njia bora ya kuzuia Urusi kuishambulia tena.