Erdogan aonya hatari ya mashambulizi Idlib
5 Septemba 2018Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan ameonya kuwa mashambulizi ya makombora na mabomu katika mkoa wa mwisho unaloshikiliwa na waasi wa Idlib nchini Syria yanaweza kusababisha maafa makubwa . Isaac Gamba anaraarifu zaidi katika taarifa ifuatayo.
Kwa mujibu wa gazeti la kila siku nchini Uturuki la Hurriyet, Erdogan amewaeleza waandishi wa habari mara baada ya kumalizika ziara yake katika jimbo la Kyrgystan barani Asia kuwa kutakuwa na mauaji makubwa kama mashambulizi ya makombora yataendelea mjini Idlib.
Matamshi hayo ya Erdogan yanakuja mnamo wakati vikosi vya Syria vikizidi kujikusanya jirani na jimbo la magharibi la Idlib kwa lengo la kufanya shambulizi kubwa ambalo tayari limeibua hofu kubwa tangu mgogoro huo ulipoanza miaka saba iliyopita.
Syria na mshirika wake mkuu Urusi wameapa kuyaondoa kabisa yale wanayoyaita makundi ya itikadi kali yanayodhibiti kwa sasa jimbo la Idlib.
Ama kwa upande wake Mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa nchini Syria Stafafan De Mistura amesema jitihada za kujaribu kuzia mapigano katika jibo la Idlib zinaendelea.
Hayo yanajiri wakati Urusi mshirika wa karibu wa rais Bashar Assad jana Jumanne ikianzisha tena mashambulizi ya anga katika jimbo la Idlib ikiwa ni baada ya kusimamisha mashambulizi hayo kwa siku 22.
Uturuki ambayo inawaunga mkono baadhi ya wapiganaji wa makundi ya waasi imekuwa ikifanya mazungumzo mara kadhaa na Urusi pamoja na Marekani yanayolenga kuzuia mashambulizi katika jimbo la Idlib.
Watu watatu wauawa Syria
Wakati huohuo kiasi ya watu watatu wameuawa na wengine 23 kujeruhiwa katika shambulizi la anga linaloshukiwa kufanywa na ndege za Israel katika maeneo ya yanayodhibitiwa na serikali ya Syria pamoja na vikosi vya Iran nchini humo.
Shirika la waangalizi wa haki za binadamu nchini Syria lenye makao yake nchini Uingereza limesema mashambulizi hayo yamefanyika katika jimbo la magharibi la Hama na katika mji wa Banias.
Shirika hilo limesema wengi wa waliojeruhiwa walikuwa ni wanajeshi wa Syria na kuwa idadi ya vifo inaweza kuongezeka kutokana na hali mbaya walionayo baadhi ya majeruhi.
Vyombo vya habari vya serikali ya Syria vimeripoti jana Jumanne kuwa mfumo wa nchi hiyo wa kujikinga dhidi ya makombora ulizuia mashambulizi ya maroketi ya Israel.
Chanzo cha habari kutoka makundi ya waasi kinasema mashambulizi hayo ya Israel yalilenga ghala la silaha la vikosi vya serikali ya Syria pamoja na washirika wake Iran.
Hata hivyo hakukuwa na taarifa rasmi kutoka Israel kuthibitisha mashambulizi hayo.
Wakati hayo yakiendelea marais wa Iran, Urusi na Uturuki wanakutana Ijumaa wiki hii mjini Tehran kawa ajili ya mkutano wa kilele kujali mstakali wa jimbo la Idlib nchini Syria.
Urusi na mshirika wake mkuu Urusi wameapa kuyaondoa kabisa makundi ya waasi yanayodhibiti kwa sasa jimbo la Idlib lakini mkutano huo wa Ijumaa huenda ukaamua ni jinsi gani mashambulizi kwenye jimbo hilo yatafanyika.
Mwandishi: Isaac Gamba/AFPE/DPAE
Mhariri : Mohammed Abdul-Rahman