Erdogan asema kulitambua taifa la Palestina ni wajibu
13 Septemba 2011Waziri mkuu wa Uturuki Tayyip Erdogan ambaye amekuwa akiikosoa sana Israel , ameuambia mkutano wa mawaziri wa mambo ya kigeni wa jumuiya ya mataifa ya Kiarabu , Arab League mjini Cairo leo, kuwa kulitambua taifa la Palestina sio suala la uchaguzi , lakini ni wajibu. Mkutano huo unajadili suala la Palestina kutaka itambuliwe na umoja wa mataifa kuwa taifa huru.
Katika hotuba ambayo itaimarisha heba yake kama kiongozi wa kimkoa, Erdogan pia ameshutumu msimamo wa Israel , akisema sera za matumizi ya nguvu, zinatishia hali ya baadaye ya watu wa Israel.
Kulitambua taifa la Palestina ni njia pekee sahihi. Sio suala la uchaguzi , bali ni wajibu. Erdogan amesema kuwa kwa mapenzi ya Mwenyezi Mungu , ifikapo mwishoni mwa mwezi huu , tutakuwa na fursa ya kuiona Palestina katika hadhi tofauti kabisa katika umoja wa mataifa. Wakati umefika wa kupandisha bendera ya Palestina katika umoja wa mataifa. Tupandishe bendera ya Palestina na bendera hiyo iwe ishara ya amani na haki katika mashariki ya kati. Tuchangie katika kupatikana amani ya kweli na uthabiti katika mashariki ya kati.
Mataifa ya Kiarabu yatataka kupatikana kwa taifa kamili la Palestina katika umoja wa mataifa wiki ijayo.
Palestina imeamua kutafuta kutambuliwa taifa lao katika umoja wa mataifa baada ya miaka kadha ya majadiliano na Israel kushindwa kuleta tija ya taifa huru ambalo wanalitaka liundwe kutokana na ardhi ya ukingo wa magharibi na ukanda wa Gaza pamoja na Jerusalem ya mashariki, maeneo ambayo yanakaliwa kimabavu na Israel baada ya vita vya mashariki ya kati vya mwaka 1967.
Erdogan , ambaye ameshuhudia umaarufu wake ukipanda katika ulimwengu wa Kiarabu kutokana na msimamo wake dhidi ya Israel, amesema kuwa sera za serikali ya Israel ni kikwazo kwa amani.Erdogan amesema.
"Israel inakuwa kama mtoto anayependa kubembelezwa. Mtazamo wake unaelekea katika hisia za taifa linaloendesha ugaidi".
Uturuki imepunguza mahusiano yake na Israel ambayo ilikuwa rafiki yake mkubwa hapo zamani kutokana na mauaji ya mwaka 2010 yaliyofanywa na makomandoo wa Israel dhidi ya wanaharakati tisa wa Kituruki katika meli zilizokuwa zinapeleka misaada katika ukanda wa Gaza. Waziri wa ulinzi wa Israel Ehud Barak hata hivyo amesema.
"Israel na Uturuki ni mataifa imara na muhimu sana katika wakati huu, katika eneo hili, na hata kama tunatofauti zetu, na tunazo nyingi, hatupaswi kuchukua hatua bila kufikiria, na bila kuwa makini".
Waziri wa mambo ya kigeni wa Qatar Sheikh Hamad bin Jassim al-Thani amesema kuwa amekuwa mwenyekiti wa mkutano huo wa Arab League na kwamba suala la Palestina ni changamoto kubwa , inayoikabili jumuiya hiyo yenye wanachama 22 .Rais wa Marekani Barack Obama amesema jana kuwa itakuwa ni hali ya kizuwizi , ambayo haitaleta manufaa yoyote ya kupatikana taifa huru, wakati Urusi imesema itawaunga mkono Wapalestina , na huku umoja wa Ulaya ukibakia umegawanyika.
Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe/rtre
Mhariri: Mohammed Abdul Rahman