1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUturuki

Erdogan ashauri kuunda tume kuchunguza mkasa wa bwawa

7 Juni 2023

Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan amependekeza kuanzishwa kwa tume ya kimataifa kuchunguza uharibifu katika bwawa la maji la Kakhovka linalodhibitiwa na Urusi kutokana na shambulizi la kombora.

Türkei Präsident Recep Tayyip Erdogan
Rais wa Uturuki Recep Tayyip ErdoganPicha: Ali Unal/AP Photo/picture alliance

Matamshi hayo ameyatoa wakati akizungumza kwa njia ya simu na marais wenzake wa Urusi na Ukraine.

Akizungumza na Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky, Rais Erdogan amesema tume hiyo inapaswa kuwajumuisha wataalamu kutoka Urusi na Ukraine, nchi hasimu ambazo zimekuwa zikitupiana lawama za uharibifu katika bwawa la kuzalisha umeme.

Pia amesema wataalamu wengine wanatakiwa wawe wa Umoja wa Mataifa na jumuia ya kimataifa ikiwemo Uturuki ili kuchunguza kwa kina shambulizi hilo.

Katika mazungumzo yake na Rais wa Urusi Vladmir Putin, Erdogan ametoa pendekezo kama hilo akisema kwamba Uturuki iko tayari kushiriki kwa sehemu yake na kwamba ni muhimu uchunguzi wa kina wa bwawa hilo lililopo katika Mto Dnipro ufanyike.

Rais Putin amesema shambulizi la kombora ni janga la kimazingira na kibinadamu na amesema ni kitendo cha kinyama, wakati ambapo, uharibifu wa bwawa hilo umesababisha maelfu ya raia kuyakimbia makaazi yao kutokana na maeneo mengi yakiwa yamefurika.

Soma pia: Maelfu waondolewa baada ya bwawa kubwa kushambuliwa Ukraine

Balozi wa Urusi katika Umoja wa Mataifa, Vasily Nebenzya, amesema shambulizi hilo lililotokea usiku wa jana limefanywa na utawala wa Ukraine na ni uhalifu usioelezeka.

''Makaazi yamefurika, maelfu ya watu wanahitaji msaada wa kuondolewa na shughuli inaendelea. Nataka kusisitiza kuwa tangu mwaka jana, uongozi wa vikosi vya kijeshi vya Ukraine ulitangaza wazi utayari wao wa kuripua bwawa hili, ili kusonga mbele kijeshi.''

Wizara ya afya ya Ukraine imeonya kuhusu kusambaa kwa magonjwa na vifo vingi vya samaki ambavyo vinaweza kusababishwa na uharibifu wa bwawa la Kakhovka.

Raia wa Ukraine wakihamishwa kwa boti baada ya kufurika kwa bwawa la Nova Kakhovka.Picha: Alina Smutko/REUTERS

Kulingana na aizara hiyo, kemikali na vimelea vya magonjwa vinaweza kuingia katika visima na vyanzo vya maji kusini mwa jimbo la Kherson kutokana na marufiko hayo. Matumizi ya samaki pia yamepigwa marufuku ili kupunguza hatari ya magonjwa.

Ama kwa upande mwingine, mashirika mbalimbali ya misaada ya Ujerumani yamepeleka misaada ya dharura nchini Ukraine kwa ajili ya watu walioathirika kutokana na uharibifu wa bwawa hilo.

Soma pia: Watu wahamishwa kufuatia shambulizi kusini mwa Ukraine

Mjini Cologne, Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuwahudumia Watoto, UNICEF limetangaza kuwa takribani watu 16,000 kutoka kwenye miji na vijiji 37 kwenye maeneo yanayodhibitiwa na serikali ya Ukraine hadi sasa wamelazimika kuhamishwa kutokana na hatari ya mafuriko.

Katika hatua nyingine, Ikulu ya Urusi, Kremlin imesema Rais Putin leo amezungumza kwa njia ya simu na kiongozi mwenzake wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa, ambapo pamoja na mambo mengine wamejadiliana kuhusu masuala yanayohusiana na juhudi za Afrika katika kutafuta suluhisho la mzozo wa Ukraine.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW