Erdogan na Netanyahu washambuliana kuhusu Gaza
2 Aprili 2018Siku ya Jumapili (1 Aprili), Rais Tayyip Erdogan wa Uturuki alimuita Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, kuwa ni "gaidi", ikiwa sehemu ya mashambulizi ya maneno makali baina yao yaliyoanza baada ya yeye Erdogan kuikosoa hatua ya kijeshi ya Israel dhidi ya maandamano katika mpaka wa Gaza.
Israel imetetea mauaji ya Wapalestina 15 wakati wa maandamano ya siku ya Ijumaa na Netanyahu alituma ujumbe kwenye ukurasa wake wa Twitter, akisema jeshi la nchi yake "halitafundishwa na watu ambao wanawapiga mabomu raia wasio hatia kwa miaka kadhaa," akikusudia Uturuki.
Lakini akizungumza na wafuasi wake hapo Jumapili, Erdogan alisema Uturuki haina aibu ya kuwa mvamizi wa mataifa mengine. "Wewe (Netanyahu) ni mvamizi na muda huu, wewe upo kwenye ardhi hizo kama mvamizi. Na wakati huo huo, wewe ni gaidi." Alisema.
Kwenye hotuba yake nyengine, Erdogan alisema: "Nyinyi ni taifa la kigaidi. Ulichokifanya Gaza kinafahamika na ulichokifanya pia Jerusalem. Hakuna anayekupenda duniani."
Baadaye akijibu mashambulizi hayo kupitia ukurasa wake wa Twitter, Netanyahu aliandika: "Erdogan hajazowea kujibiwa, lakini anapaswa aanze kujitayarisha. Yeye ambaye anaikalia Cyprus kaskazini, anayenyemelea mamlaka ya Wakurdi na mauaji ya maangamizi ya Afrin hawezi kutuhubiria sisi juu ya maadili na miiko."
Israel yakataa wito wa uchunguzi
Hayo yakiendelea, Waziri wa Ulinzi wa Israel, Avigdor Lieberman, amekataa wito wa kufanyika uchunguzi huru juu ya mauaji hayo ya Gaza, akisema "maandamano hayo hayakuwa tamasha la kuni."
Liberman, anayetambuliwa kuwa mfuasi wa siasa kali za Kiyahudi, amesema miito hiyo ya uchunguzi huru ni ya kinafiki.
"Hakutakuwa na kamisheni yoyote ya uchunguzi. Hapatakuwa na kitu kama hicho hapa.
Hatutashirikiana na kamisheni yoyote ya uchunguzi," alikiambia kituo kimoja cha redio ya umma nchini mwake siku ya Jumapili.
Jeshi la Israel linakabiliwa na ukosoaji mkali kutoka makundi ya haki za binaadamu juu ya matumizi yake ya silaha za moto dhidi ya waandamanaji siku ya Ijumaa, siku inayotajwa kuwa ya mauaji mabaya kabisa kwenye mzozo wa Gaza na Israel tangu vita vya mwaka 2014, huku Wapalestina wakiwatuhumu wanajeshi kwa kuwapiga risasi waandamanaji ambao hawakuwa na kitisho chochote.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, na Mkuu wa Sera za Nje wa Umoja wa Ulaya, Federica Mogherini, wametaka kufanyika kwa uchunguzi huru, lakini siku ya Jumamosi, Marekani ilizuwia rasimu ya tamko la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ambalo lingelikuwa linatoa wito wa pande zote mbili kujizuwia na wakati huo huo likiitisha uchunguzi huo.
Mwandishi: Mohammed Khelef/Reuters/AFP
Mhariri: Daniel Gakuba