1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Erdogan: Uongozi wa juu Saudia ulipanga mauaji ya Khashoggi

3 Novemba 2018

Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan amesema amri ya kumuua Jamal Khashoggi ilitoka kwa "watu wa ngazi ya juu" katika serikali ya Saudi Arabia huku akiapa kutokata tamaa katika juhudi za kuwasaka waliomuua.

Erdogan bei AKP-Sitzung
Picha: Reuters/Presidential Press Office/M. Cetinmuhurdar

Akizungumza jana, ikiwa ni mwezi mmoja baada ya Khashoggi kuuawa katika ubalozi mdogo wa Saudia mjini Istanbul, Erdogan amesema haamini hata kidogo kuwa Mfalme Salman anapaswa kulaumiwa.

Lakini alishindwa kumuondolea lawama Mwanaflame mrithi Mohammed bin Salman kwa kumtumia kikosi cha wauwaji mwanahabari huyo wa Saudia ambaye kifo chake kimeichafua hadhi ya kiongozi huyo.

Mwili wa Khashoggi bado haujapatikanaPicha: picture-alliance/abaca/Depo Photos

Katika tahariri ya gazeti la Washington Post, ambalo Khashoggi alikuwa mchangiaji, Erdogan amewatuhumu maafisa wa Saudia kwa kukataa kujibu maswali muhimu kuhusu mauaji hayo licha ya kuwakamata washukiwa 18.

Lakini amesema serikali yake itaendelea kuuliza maswali mengine "maafisa wa Saudia wamekataa kujibu,” kama vile ni wapi uliko mwili wa Khashoggi na ni nani aliyeamuru auliwe.

Mauaji hayo ya Khashoggi aliyekuwa mkosoaji mkubwa wa ufalme wa Saudia, umechochea kilio na shutuma kali kutoka Marekani, ambaye kawaida huwa mshirika mkubwa wa taifa hilo la Kifalme.

Wakati Rais Donald Trump amefuta uwezekano wa kusitisha mkataba wa mauzo ya silaha na Saudia kama adhabu, utawala wake umeondoa uungwaji mkono kwa vita vya muungano wa kijeshi unaongozwa na Saudia nchini Yemen.

Akiwahutubia waombolezaji katika ibada ya kumbukumbu mjini Washington Ijumaa, mchumba wa mwanahabari huyo aliyeuawa alimuomba Trump kuunga mkono juhudi za Uturuki kuchunguza kifo chake.

Mchumba wake anaitaka Marekani isaidie uchunguziPicha: Reuters/Haberturk

"Ningependa kutuma ujumbe huu kwa Bwana Trump: Ningependa aunge mkono juhudi za kisheria za Uturuki katika kujaribu kupata ukweli wa mambo na kupata uliko mwili wake,” Alisema Hatice Cengiz katika ujumbe uliorekodiwa.

Mwendesha mashitaka mkuu wa Uturuki amesema wiki hii kuwa Khashoggi alinyongwa mara tu baada ya kuingia katika ubalozi huo mdogo na pia akathibitisha kuwa mwili wake ulikatwa katwa kwenye vipande.

Yasin Aktay, mshauri wa Erdogan, alidokeza kwenye Makala iliyochapishwa Ijumaa kuwa mwili wake huenda hata uliharibiwa kwenye tindikali.

"Sasa tunaona kuwa haukukatwakatwa tu, waliuharibu kwa kuuyeyusha”, alisema afisa huyo wa chama tawala, katika gazeti la Hurriyet.

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu, ambaye nchi yake pamoja na Saudia zinaendeleza uhasama dhidi ya Iran,amelaani mauaji hayo lakini akasisitiza kuhusu haja ya kuwepo utulivu nchini Saudi Arabia.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW