Erdogan: Vikosi vya Uturuki vimemuua Kiongozi wa IS
1 Mei 2023Katika mahojiano na kituo cha televisheni cha Uturuki ,TRT, hapo jana, Erdogan alithibitisha kuwa kiongozi huyo anayefahamika kwa jina la Abu Hussein al-Qurayshi, aliuawa katika operesheni iliyofanyika siku ya Jumamosi.
Erdogan alisema idara ya ujasusi ya Uturuki, MIT, ilikuwa ikimfuatilia al-Qurayshi kwa muda mrefu na kusisitiza:
"Mungu akituwezesha, tutaendeleza mapambano makali dhidi ya makundi yote ya kigaidi bila kuliacha nyuma hata moja."
Soma pia: Kiongozi wa Dola la Kiislamu Syria auliwa
Hata hivyo, kundi la IS halijathibitisha taarifa hii. Uturuki imekuwa ikifanya operesheni kadhaa dhidi ya kundi hilo na dhidi ya wanamgambo wa Wakikurdi katika mpaka wake na Syria. Operesheni hizo hupelekea kukamatwa au kuuawa kwa wale wanaoshukiwa kuwa wapiganaji.
Uturuki inadhibiti maeneo makubwa ya kaskazini mwa Syria kufuatia msururu wa mashambulizi inayodai ni kwa ajili ya kuyafurusha makundi ya Wakurdi mbali na mpaka wake na Syria.
Abu Hussein al-Qurayshi alitangazwa kuwa kiongozi wa kundi la IS baada ya kiongozi wa awali, Abu Bakr al-Baghdadi, kuuawa kaskazini-magharibi mwa Syria mwezi Oktoba mwaka 2019 na vikosi vya Marekani.
Soma pia: Trump athibitisha kifo cha kiongozi wa "Dola la Kiislamu"
Mrithi wake, Abu Ibrahim al-Hashimi al-Qurayshi, aliuawa katika shambulio sawa na hilo mwezi Februari mwaka 2022. Alifuatiwa na Abu al-Hassan al-Hashimi al-Quraishi, ambaye kwa mujibu wa jeshi la Marekani aliuawa pia katikati ya mwezi wa Oktoba katika operesheni ya waasi wa Syria katika jimbo la kusini mwa nchi hiyo la Daraa.
Viongozi wote hao wa kundi la IS kupewa jina la al-Quraishi haimanishi kuwa wana uhusiano wowote wa udugu bali, ni jina la kivita linalotokana na kabila la Mtume Muhammad.
Msemaji wa IS aliwahi kumtaja al-Qurayshi kuwa ni mmoja wa mashujaa wa vita na mmoja wa wana waaminifu wa kile kinachoitwa Dola la Kiislamu.
Kiongozi huyo na historia ya kundi la IS
Al-Qurayshi alichukua uongozi wa IS wakati kundi hilo la itikadi kali za kiislamu lilikuwa limepoteza udhibiti wa maeneo ambayo hapo awali lilikuwa likiyadhibiti nchini Iraq na Syria. Walakini, alijaribu kulifufua kundi hilo na kufanya mashambulizi mabaya katika nchi zote mbili.
Kundi linalojiita Dola la Kiislamu IS lilijitenga na kundi la al-Qaida takriban muongo mmoja uliopita na hatimaye kudhibiti sehemu kubwa za kaskazini na mashariki mwa Syria na kaskazini na magharibi mwa Iraq.
Soma pia: Jeshi la Syria lapokea sifa kwa kumuuwa kiongozi wa IS
Mnamo mwaka 2014, IS walitangaza kinachojulikana kama "Khalifa" yaani kiongozi wa umma, na hivyo kuwavutia wafuasi wengi kutoka pande zote za dunia.
Katika miaka iliyofuata, walidai kuhusika katika mashambulizi kadhaa duniani kote ambayo yalisababisha vifo na kujeruhi mamia ya watu kabla ya wao kushambuliwa pia kila kona hadi kunyakuliwa sehemu zote walizokuwa wakizidhibiti.