Eriksen kuwekewa kifaa cha kufuatilia mapigo ya moyo
17 Juni 2021Eriksen anaendelea kupata nafuu hospitalini mjini Copenhagen baada ya kupata mshtuko wa moyo wakati wa mechi ya ufunguzi ya timu ya taifa ya Denmark dhidi ya Finland katika michuano ya kombe la EURO 2020. Soma zaidi Mechi ya Denmark na Finland EURO 2020 yaanza tena
Shirikisho la Soka la Denmark limesema madaktari wamegundua kuwa Eriksen anahitaji kifaa kinachotambulika kitaalamu kama implantable cardioverter-defibrillator (ICD).
''Kifaa hiki ni muhimu baada ya mshtuko wa moyo kwa sababu ya usumbufu wa mapigo ya moyo, Christian amekubali suluhisho hilo na mpango huo umethibitishwa na wataalamu kitaifa na kimataifa ambao wote wanapendekeza matibabu sawa. Tunamuhimiza kila mtu kumpa Christian na familia yake amani na faragha wakati huu," shirikisho la Denmark limesema katika taarifa.
Kifaa cha ICD kinafuatilia mapigo ya moyo na kinaweza kutuma mapigo ya umeme kurudisha mapigo ya moyo ya kawaida inapohitajika.
Kiungo mkabaji wa Uholanzi Daley Blind pia amepandikiziwa kifaa hicho cha ICD na bado anacheza soka la kulipwa. Blind aliwekewa kifaa hicho baada ya kugunduliwa na tatizo la misuli ya moyo mwaka 2019.
Denmark Alhamisi inashuka dimbani kuchuana na Ubelgiji. Dakika 10 baada ya mechi kuanza mechi hiyo itasimamishwa kwa dakika moja kupiga makofi ya heshima kwa Eriksen, dakika ya kumi ya mchezo kama nambari ya jezi yake ya timu ya taifa.
AP