1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Eritrea kuondosha wanajeshi wake Ethiopia

26 Machi 2021

Baada ya serikali ya Ethiopia kukiri kuwepo kwa wanajeshi wa Eritrea kwenye jimbo la kaskazini la Tigray, sasa Waziri Mkuu Abiy Ahmed ametangaza kwamba wanajeshi hao wa taifa jirani sasa wanaondoka.

Äthiopien Premierminister Abiy Ahmed Parlament
Picha: Yohannes Gebireegziabher/DW

Taarifa yake hiyo ya Ijumaa (Machi 26) inafuatia ziara fupi aliyoifanya mjini Asmara, mji mkuu wa Eritrea, kukutana na uongozi wa huko.

Wanajeshi wa pande zote mbili, Ethiopia na Eritrea, wanatuhumiwa kutenda vitendo vingi vya ukatili dhidi ya raia kwenye jimbo la Tigray lililo mpakani mwa nchi hizo mbili.

"Kufuatia majadiliano yangu ya leo Ijumaa na Rais Isaias Afwerki wa Eritrea, serikali ya Eritrea imekubali kuondowa wanajeshi wake kwenye mpaka wa Ethiopia", alisema Abiy kupitia mtandao wa Twitter.

Hata hivyo, kuna tetesi kwamba wanajeshi wa Eritrea hawako tu eneo la mpakani, bali wameingia ndani kabisa ya ardhi ya Ethiopia lakini haifahamiki ikiwa nao pia wataondoka kupitia tangazo hilo la Waziri Mkuu Abiy Ahmed.

Kwa mara ya kwanza, mshindi huyo wa Tuzo ya Amani ya Nobel alikiri kuwepo kwa wanajeshi wa Eritrea kwenye jimbo la Tigray siku ya Jumanne (Machi 23), baada ya miezi kadhaa ya kukanusha taarifa za wakaazi wa huko, wanadiplomasia na hata za baadhi ya maafisa wa kijeshi juu ya kuwepo kwao.

Jeshi la Eritrea lilivyoingia Ethiopia

Abiy aliamuru wanajeshi kuingia Tigray mnamo tarehe 4 Novemba, baada ya kuwatuhumu wapiganaji wa Chama cha Ukombozi wa Watu wa Tigray (TPLF) kuishambulia kambi ya jeshi la Ethiopia. 

Jeshi la Ethiopia wakati wa kuingia jimbo la Tigray tarehe 16 Novemba 2020.Picha: Ethiopian News Agency/AP/picture alliance

TPLF iliwahi kuwa chama tawala nchini Ethiopia na ndiyo iliyoongoza vita kati ya nchi hiyo na Eritrea, ambavyo vilizusha uhasama wa muda mrefu baina ya mataifa hayo yaliyowahi kuwa nchi moja. 

Mnamo mwaka 2018, Abiy Ahmed alifanikiwa kufikia makubaliano ya amani na Eritrea, kitendo ambacho kilimuwezesha kutunukiwa Tuzo ya Amani ya Nobel.

Lakini tangu wakati huo, waziri mkuu huyo amekuwa akituhumiwa kushirikiana na vikosi vya Eritrea kuwaandama viongozi wa TPLF, ambao kwa sasa wamekimbia na hawajulikani walipo.

Mashahidi wanasema kwamba wanajeshi wa Eritrea walikuwepo Tigray tangu mwanzoni mwa mapigano kati ya jeshi la Ethiopia na TPLF, kinyume na taarifa ya Abiy, kwamba waliingia baada ya vita kuanza ili kulinda mpaka wao.

Mashirika ya haki za binaamu ya Amnesty International na Human Rights Watch yanawashutumu wanajeshi wa Eritrea kufanya mauaji ya kimbari dhidi ya mamia ya Watigray katika mji wa Axum.

Wanajeshi wa Ethiopia pia wanatuhumiwa kwa utesaji na  mauaji, ambapo hapo jana Shirika la Madktari Bila Mpaka, MSF, lilisema wafanyakazi wake walishuhudia wanajeshi hao wakiuwauwa wanaume wanne mbele ya macho yao na kuwatesa wengine kadhaa.
 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW