Eritrea yaanzisha uhusiano wa kidiplomasia na Somalia
30 Julai 2018Ziara ya siku tatu ya rais wa Somalia Mohamed Abdullahi Mohammed mjini Asmara nchini Eritrea inaingiliana na hatua ambayo si ya kawaida ya hatua za amani baina ya Eritrea na Ethiopia , sehemu ya mabadiliko ya kushangaza katika eneo hilo ambalo lilikabiliwa na vita , mizozo inayowahusu mahasimu ambayo inachochewa katika nchi nyingine , kutengwa na utawala wa mkono wa chuma.
"Nchi hizo mbili zitaanzisha mahusioano ya kidiplomasia na kubadilishana mabalozi," imeeleza tamko la "pamoja kuhusu uhausiano wa kindugu" lililotiwa saini mjini Asmara na rais wa Eritrea Isaias Afwerki na Mohammed wa Somalia.
Tamko hilo limekuja kiasi wiki tatu baada ya Ethiopia na Eritrea kutangaza mwisho wa miongo miwili ya mzozo wao, na kurejesha mahusiano ya kidiplomasia kwa haraka na safari ya anga kati ya miji yao mikuu.
Historia ya mataifa hayo matatu , na mtengano wao , vinakwenda pamoja. Somalia na Eritrea zilikuwa mwanzo karibu. Chini ya dikteta wa somalia siad Barre , utawala wa kijeshi mjini Mogadishu uliunga mkono mapambano ya muda mrefu ya kudai uhuru kutoka Ethiopia, ambao waliupata mwaka 1993.
Mwaka 1998 Ethiopia na Eritrea zilianza kupigana vita vya miaka miwili kuhusiana na suala la mpaka wao ambavyo vilisababisha watu 80,000 kupoteza maisha kabla ya kuingia katika vita vikali baridi.
Vita vya kihasama
Baada ya kuanguka kwa utawala wa Barre mwaka 1991, Somalia ilitumbukia katika machafuko na vurugu.
Ilipofika mwaka 2006 , Somalia iligeuka kuwa eneo kama wachunguzi wanavyosema la vita baina ya Eritrea na Ethiopia.
Ethiopia ikiunga mkono serikali dhaifu ya mpito mjini Mogadishu wakati Eritrea ilishutumiwa kuunga mkono wanamgambo wa Kiislamu wanaopigana kuiangusha serikali , madai ambayo inayakana.
Baraza la Usalama la Umoja wa mataifa mwaka 2009 liliweka vikwazo vya silaha na vikwazo vilivyowalenga baadhi ya viongozi dhidi ya Eritrea kwa madai ya kwamba inaunga mkono kundi la Kiislamu lenye mahusiano na wanamgambo wa al-Shabaab , ambalo liliendelea kufanya mashambulizi yake ya mara kwa mara licha ya kupoteza maeneo katika miaka ya hivi karibuni.
Tamko hilo rasmi la pamoja limeweka msisitizo maalum katika uungaji wake mkono kwa serikali ya Somalia.
"Eritrea inaunga mkono kwa dhati uhuru wa kisiasa, uhuru na mipaka ya Somalia pamoja na juhudi za watu na serikali ya Somalia kurejesha hadhi halali ya nchi hiyo na kufanikisha matarajio ya watu wake," limesema tamko hilo. Waraka huo , uliowekwa katika tovuti ya wizara ya habari ya Eritrea , pia umesema mataifa hayo mawili, " yatafanya jitihada kutengeneza ushirikiano wa kisiasa, kiuchumi, kijamii, kitamaduni pamoja na ulinzi na usalama.
Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe
Mhariri: Yusuf Saumu