Eswatini yapiga marufuku maandamano
22 Oktoba 2021Waziri wa Kazi ya Umma nchini humo Prince Simelane amewaambia waandishi wa habari kwamba kufuatia misururu ya visa vya vurugu katika maandamano hayo, amewaamuru wakuu wa manispaa ya miji kutotoa idhini ya maandamano.
Mnamo siku ya Alhamisi, muandamanaji mmoja alifariki hospitalini kutokana na jeraha la risasi alilopata baada ya kushambuliwa siku ya Jumatano wakati maafisa wa polisi walifyatua risasi dhidi ya waandamanaji. Hayo ni kulingana na vyama vya wafanyakazi.
Soma: Amnesty Int: Ufalme wa Eswatini uache kukandamiza wakosoaji
Chama cha wauguzi kimesema wahudumu wa afya wasiopungua 30 pia walipata majeraha ya risasi na wanatibiwa. Mnamo siku ya Alhamisi, wafanyakazi wa shirika la reli waliongoza maandamano mapya katika taifa hilo la kifalme ambalo awali liliitwa Swaziland.
Intaneti na mitandao ya kijamii yasuasua
Huduma za intaneti nchini humo zimekuwa chini huku mtandao wa Facebook ukizimwa kabisa kwa siku ya pili mfululizo.
Jeff Radebe ambaye ni mkuu wa wapatanishi wa kikanda ambao wametumwa na Jumuiya ya Kimaendeleo ya nchi za kusini mwa Afrika SADC, ameliambia shirika la habari linalomilikiwa na serikali ya Afrika Kusini kwamba, picha ya hali ilivyo nchini Eswatini ni za kusikitisha, na kwamba joto la kisiasa nchini humo liko juu zaidi.
Soma: Jeshi latumwa kuwatuliza wanafunzi wanaoandamana Eswatini
Kupitia taarifa, chama cha wauguzi nchini Eswatini kimesema wauguzi pamoja na wahudumu wengine wa afya waliojitokeza kuandamana katika bustani ya Mbabane walikabiliwa na nguvu nyingi ya kupindukia kutoka kwa maafisa wa polisi pamoja na jeshi.
Vikosi vya usalama vyashutumiwa kutimia nguvu nyingi
Taarifa hiyo imezidi kueleza kwamba walitawanywa kwa nguvu na walipokuwa wakikimbia walipigwa risasi. Wale 30 waliotibiwa walikuwa miongoni mwa zaidi ya 80 walioripotiwa kujeruhiwa siku ya Jumatano wakati wa maandamano hayo ya taifa zima kushinikiza demokrasia.
Radebe amehoji kwamba masuala yanayolikumba taifa hilo ni tete na timu yake inaelekea nchini humo tayari kusikiliza pande zote ili mwisho wa yote, watu wa Eswatini wapate suluhisho la kudumu.
Soma: HRW yaitaka Eswatini kuheshimu haki za raia
Maandamano ya hivi karibuni ambayo yamedumu kwa zaidi ya wiki mbili sasa, yalianzishwa na wanafunzi, wafanyakazi wa umma pamoja na wafanyakazi katika sekta ya uchukuzi.
Mfalme Mswati wa tatu ndiye mfalme wa mwisho kabisa mwenye mamlaka ya utawala wa nchi barani Afrika, na amekuwa akijifurahisha kwa utajiri wake na kuwapa wake zake 15 zawadi nyingi za thamani. Ilhali anaongoza moja kati ya nchi maskini zaidi ulimwenguni kote ambako takriban theluthi mbili ya raia wote wanaishi maisha ya ufukara na robo ya watu wameambukizwa virusi vya ukimwi.
Hali hospitalini sawa na 'hali katika eneo la vita'
Kupitia taarifa, chama cha Kikomunisti cha Swaziland kimesema mnamo siku ya Jumatano, hali katika hospitali kubwa zaidi ya serikali iliyoko Mbabane ilifanana na ‘hali ya eneo la vita'.
Soma: Maandamano ya kupinga utawala wa eSwatini yageuka na kuwa vurugu
Sakafu zilitapakaa damu na polisi walivamia pia hospitali na kuwapiga wauguzi risasi walipokuwa wakiwahudumia majeruhi, hatua iliyofanya hali kuwa mbaya zaidi.
Chama cha wauguzi kimesema vikosi vya polisi viliendelea kuwapiga risasi wauguzi usiku hata walipokuwa wakisafiri kuenda hospitalini kufanya kazi usiku. Kwa kughadhabishwa na kitendo hicho, chama hicho kimetoa wito kwa wauguzi na wahudumu wa afya kutowatibu wanajeshi na polisi ambao wamejeruhiwa.
Mnamo siku ya Alhamisi, wanafunzi watano wa shule ya sekondari waliokamatwa wakati wa maandamano walifunguliwa mashtaka ya ugaidi kufuatia ushiriki wao kwenye maandamano hayo. Waendesha mashtaka waliwatuhumu kwa kuchoma moto kituo cha polisi.
Watu wasiopungua 30 wamefariki tangu mwezi Juni kufuatia maandamano hayo mabaya kuwahi shuhudiwa katika historia ya taifa hilo la kusini mwa Afrika.
(AFPE)