Mtetezi wa haki Daniel Bekele akosolewa kwao Ethiopia
18 Novemba 2021Mapigano yanayoendelea kati ya vikosi vya Ethiopia na wanamgambo wa TPLF, chama ambacho kiliwahi kuongoza serikali ya Ethiopia, yamesababisha vifo vya maelfu ya watu na wengine wapatao milioni mbili kupoteza makazi yao tangu mwezi Novemba 2020.
Soma zaidi: Ndege za Ethiopia zashambulia maeneo mawili jimboni Tigray
Kulingana na Daniel Bekele, pande zote zinahitaji kuwajibishwa kwa ukatili uliofanywa wakati wa vita.
Kwa kujitolea kwake kutetea haki za binadamu na kupinga dhuluma, Ujerumani ilimtunuku Daniel Bekele Tuzo ya Afrika ya 2021. Tuzo hiyo ya aina yake inawatambua Waafrika mashuhuri ambao wamejitolea kupigania amani, upatanisho na maendeleo ya kijamii.
Serikali ya zamani ya EPRDF ilimkamata na kumuweka kizuizini Daniel mwaka 2005, baada ya kuukosoa uchaguzi uliokuwa na utata wa mwaka huo. Wakati huo, chama cha TPLF kilikuwa na ushawishi mkubwa katika serikali ya mseto iliyokuwa madarakani. Lakini kabla ya kuwekwa kizuizini, alipigwa vibaya na watu wasiojulikana. Aliachiliwa huru miaka miwili na nusu baadae, na kuchaguliwa kama Mkurugenzi wa kitengo cha Afrika cha shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch mnamo mwaka 2011.
Nilikulia wakati wa uongozi wa kidikteta wa kijeshi na ambapo watu wengi waliwekwa kizuizini kiholela, wengine waliuliwa, kupigwa, na kuteswa vibaya, Daniel aliiambia DW.
"Nimeshuhudia baba yangu na mama yangu wakiwekwa kizuizini. Na kisha udikteta huo wa kijeshi ukapinduliwa na vuguvugu la waasi wenye silaha, na ikaanza enzi ya matumaini, lakini iliishia katika kipindi kingine cha ukandamizaji wa kisiasa."
Na mwaka 2019, Waziri Mkuu Abiy Ahmed alimteua Daniel kuiongoza tume ya haki za binadamu ya Ethiopia.
Bekele adaiwa kuipendelea serikali ya Abiy Ahmed
Chini ya uongozi wake, tume hiyo ilikosolewa vikali hususan na TPLF, kwa kuipendelea serikali ya Abiy. Wakosoaji wake wanadai kwamba Daniel hataweza kutokuwa na upendeleo katika mzozo wa Ethiopia kwa sababu aliwahi kukamtwa na TPLF.
Vidio iliyowekwa Youtube na wakosoaji wa serikali ya Abiy inadai kwamba Daniel aliiunga mkono serikali wakati wa maamndamano ya Oromo ya mwaka 2020, kufuatia mauaji ya mwanamuziki Hachalu Hundessa.
Serikali iliyazima maandamano hayo kwa kutumia nguvu ya kupindukia. Vidio hiyo inasema Daniel aliitetea serikali kuwa ina haki ya kurejesha amani na utulivu kwenye eneo hilo. Watu wapatao 160 waliuliwa kwenye maandamano hayo yaliyokuwa na vurugu, kulingana na shirika la Amnesty International.
Hata hivyo kuna waliosema Daniel pia aliukosoa upande wa serikali. Kwa mfano tume yake ilichapisha ripoti iliyoeleza ukiukwaji wa haki za binadamu uliotendwa katika maeneo tofauti ya Ethiopia mwezi Mei. Uchunguzi huo ulitahadharisha juu ya hali mbaya katika vituo vya polisi vya jimbo la Oromia lenye idadi kubwa ya watu na pia alikozaliwa Waziri Mkuu Abiy Ahmed.
Mapema mwaka huu, Marekani imedai kuwa kinachoendelea katika jimbo la Tigray ni kujaribu kulitokomeza kabila hilo, madai ambayo serikali ya Abiy inayakana.
Mnamo mwezi Novemba, serikali ya Ethiopia ilitangaza hali ya hatari nchini kote. Hatua hiyo inawapa maafisa wa usalama fursa ya kuwakamata kiholela watu wanaowashuku, huku waangalizi wengi wakihofia kuwa hali hiyo inaweza kuhalalisha zaidi ukiukaji wa haki za binadamu.
Lakini Daniel anasisitiza kwamba ataendelea kuukosoa kila upande utakaokiuka haki za binadamu.