1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ethiopia, Eritrea zaanza mazungumzo ya ngazi za juu

Oumilkheir Hamidou
26 Juni 2018

Ujumbe wa ngazi ya juu wa serikali ya Eritrea unatarajiwa kuwasili katika nchi jirani ya Ethiopia kwa mazungumzo kuhusu juhudi za amani na kufufua matumaini ya kumalizika ugonvi uliodumu muda mrefu kabisa barani Afrika.

Rais Isaias Afewerkii wa Eritrea
Rais Isaias Afewerkii wa EritreaPicha: Eritrea Minister of Information/Y.G. Meskel

Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed alisema mapema mwezi huu yuko tayari kutekeleza masharti yote ya makubaliano ya amani  ya mwaka 1998-2000 yaliyomaliza ugonvi wa nchi hizo mbili, akiashiria uwezekano wa kupatiwa ufumbuzi mvutano kuhusu mpaka wa nchi hizo mbili.

Rais Isaias Afwerki wa Eritrea akasema wiki iliyopita, anakaribisha kile alichokiita "risala za maana" kutoka Ethiopia na kuamua kutuma ujumbe wa kwanza rasmi wa serikali yake kuwahi kwenda Addis Abeba baada ya kupita miongo miwili .

Ujumbe wa Eritrea unawaleta pamoja mshauri wa rais Yemane Gebreab, waziri wa mambo ya nchi za nje Osman Saleh na mwakilishi wa Eritrea katika Umoja wa Afrika-hayo ni kwa mujibu wa kituo cha matangazo kinachomilikiwa na serikali nchini Ethiopia.

Wanajeshi wa Eritrea katika eneo la mpakaniPicha: Getty Images/AFP/S. Forrest

Hali ya kutoaminiana imetanda bado kati ya pande mbili

Eritrea na Ethiopia zilipigana vita vya mpakani vilivyoangamiza maisha ya watu wasiopungua 80.000.Nchi hizo mbili zinaendelea kuzozana kuhusiana na kanuni za mji wa mpakani wa Badme.Tangu wakati ule wanajeshi wamewekwa katika eneo hilo la mpakani. Kila mmoja hamuamini mwenzake anasema  mwandishi habari wa kujitegemea Martin Plaut katika mahojiano na DW:

"Ni tukio la maana baada ya miaka 20 ya uhusiano baridi ambao mtu hawezi kuulinganisha na uhusiano wa amani wala wa vita. Malaki wametawanyika kutokana na mvutano huo na baadhi ya wakati risasi zikifyetuliwa mpakani. Kwa hivyo tukio lolote litakalomaliza hali hiyo ya mvutano linakaribishwa. Bila ya shaka njia ni ndefu na kizingiti kikubwa ni jinsi ya kuaminiana kwasababu baada ya muda mrefu wa mvutano kila upande unamwangalia mwenzake kwa jicho la tahadhari.

Ujumbe wa kwanza wa Eritrea kuingia Ethiopia

Eritrea na Ethiopia zimevunja uhusiano wa kidiplomasia tangu miongo miwili iliyopita ingawa serikali ya mjini Asmara ina mwakilishi wa kudumu katika Umoja wa Afrika mjini Addis Abeba-mji mkuu wa Ethiopia.

Hakuna mwakilishi yeyote wa serikali ya Eritrea aliyewahi kushiriki katika mazungumzo yoyote rasmi pamoja na viongozi wa serikali ya Ethiopia tangu mwaka 1998.

 

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Reuters

Mhariri: Iddi Ssessanga

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW