Ethiopia, Eritrea zafanya mkutano wa kihistoria
9 Julai 2018Tangazo hilo limehitimisha wiki kadhaa za wimbi la mabadiliko, lililoongozwa na Abiy, wakati ambapo alizuru katika mji mkuu wa Eritrea kwa ajili ya mazungumzo ya ana kwa ana na Afwerki.
Akizungumza wakati wa hafla ya chakula cha jioni kilichoandaliwa na Rais wa Eritrea Isaias Afwerki, Waziri mkuu wa ETHIOPIA Abiy Ahmed alisema wamekubaliana kwamba mashirika ya ndege yataanza kuhudumu, bandari zitafunguliwa, watu wataweza kuingia na kutoka katika nchi hizo mbili na balozi pia zitafunguliwa. Amesema "Ukuta ambao ulijengwa katikati ya watu wetu dhidi ya mapenzi yao kwa miaka 20 unahitaji kubomolewa. Vita vilivyowaua maelfu ya watu na kutupotezaa miaka mingi na kutusababishia hasara kubwa kiuchumi iligeuka kuwa vita bila kifo".
Mataifa hayo ya pembe ya Afrika yamekuwa yakizozana tangu Ethiopia ilipokataa uamuzi wa Umoja wa Mataifa na kukataa kuwachia ardhi ya Eritrea kwenye mpaka wa nchi hizo kufuatia vita vya kati ya mwaka 1998 hadi 2000 ambavyo viliwauwa watu 80,000.
Kiongozi wa muda mrefu wa Eritrea Isaias Afwerki alimkaribisha Abiy katika uwanja wa ndege wa Asmara kabla ya kuelekea katika Ikulu kwa ajili ya mazungumzo yaliyodumu siku nzima.
Viongozi hao wawili walipeana mikono na kukumbatiana kabla ya kuondoka katika uwanja wa ndege wakishangiliwa barabarani na maelfu ya Waeritrea ambao walipeperusha bendera za Ethiopia na Eritrea. Afwerki alimpongeza Abiy kwa juhudi zake za kuleta amani "Hakika hisia walizoonesha watu leo zinadhihirika wazi. Fursa zilikuwepo na tulitaraji kuzitumia vyema, lakini ziliwekwa mbali na sisi katika miaka 25 iliyopita" Alisema Afwerki.
Kurejeshwa kwa mahusiano ya kidiplomasia na kibiashara baada ya miaka mingi ya uhasama mkali huenda kukaleta manufaa makubwa kwa mataifa yote mawili, na eneo zima la Pembe ya Afrika, linalokumbwa na migogoro na umaskini.
Eritrea ambayo wakati mmoja ilikuwa mkoa wa Ethiopia ambao ulikuwa na mwambao wa pwani katika Bahari ya Shamu, ilipiga kura kujitenga katika mwaka 1993, baada ya miongo kadhaa ya mapambano makali ya kupigania huru. Kujitenga huko kuliifanya Ethiopia kuwa nchi isiyokuwa na bandari na kudorora kwa mahusiano kutokana na vita baridi kukaifanya Ethiopia kuitegemea Djibouti kwa ajili ya kufanya biashara zake za bandarini.
Hatua ya Ethiopia kuruhusiwa tena kuzitumia bandari za Eritrea itapiga jeki uchumi wa hizo mbili, pamoja na kuipa changamoto kutanuka kunakoongezeka kwa Djobouti ambayo ilifaidika kwa kununua na kuuza bidhaa nyingi katika taifa hilo la pili kwa idadi ya watu barani Afrika.
Uhamiaji huru wa mpakani pia utaziunganisha, kwa mara nyigine, watu wa nchi hizo mbili ambao wanaunganishwa na historia, lugha na kabila.
Mwandishi: Bruce Amani/AFP
Mhariri: Josephat Charo