1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ethiopia ina wasiwasi juu ya Misri kupeleka silaha Somalia

24 Septemba 2024

Ethiopia imeelezea wasiwasi wake kuhusu Misri kupeleka shehena ya silaha nchini Somalia. Kwa upande wake eneo linalojitawala la Somaliland limesema silaha hizo zinaweza kuingia kwenye mikono mibaya.

Abiy Ahmed Ali | Waziri Mkuu wa Ethiopia
Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed AliPicha: Massimo Percossi/Ansa/ZUMA Press/IMAGO

Waziri wa mambo ya nje wa Ethiopia Taye Astke Selassie, amesema nchi yake ina wasiwasi kwamba silaha zinazopelekwa Somalia zitaishia kwenye mikono ya magaidi.

Shirika la habari la umma nchini Ethiopia limeripoti kwamba Meli ya kivita ya Misri ilitia nanga mjini Mogadishu kwa ajili ya kuterenmsha shehena ya pili ya silaha kwa Somalia. Miongoni mwa silaha hizo ni zile za kudungua ndege na mizinga.

Waziri wa mambo ya nje wa Ethiopia Taye Astke SelassiPicha: Solomon Muchie/DW

Meli ya kivita ya Misri ilianza kushusha silaha hizo siku ya Jumapili. Mwanadiplomasia mmoja amesema, vikosi vya usalama viliweka ulinzi kando ya barabara tangu siku hiyo ya Jumapili na jana Jumatatu wakati misafara ya magari ilizisafirisha silaha hizo hadi kwenye jengo la wizara ya ulinzi na kambi za kijeshi zilizo karibu.

Soma: Somalia na Ethiopia zafanya mazungumzo nchini Uturuki 

Wizara ya mambo ya kigeni ya eneo linalojitawala la Somaliland imesema katika taarifa yake kwamba eneo hilo lina wasiwasi kwamba silaha hizo zinaweza kuingia katika mikono isiyo salama kama vile kwa wapiganaji wa kundi la al- Shabaab lenye uhusiano na kundi la kigaidi la al-Qaeda.

Uhusiano kati ya Misri na Somalia umeongezeka mwaka huu baada ya nchi hizo kutia saini mkataba wa pamoja wa usalama mnamo mwezi Agosti, kutokana na kwamba nchi hizo hazina mahusiano mema na Ethiopia.

Ethiopia iliikasirisha Somalia baada ya kufikia makubaliano ya awali mnamo mwezi Januari na Somaliland juu ya kukodisha bandari yake kwa Ethiopia na kisha nchi hiyo iutambue uhuru wa Somaliland kutoka Somalia.

Bandari ya Barbera katika eneo la SomalilandPicha: Eshete Bekele/DW

Somalia imesisitiza kwamba mkataba kati ya Ethiopia na eneo la Somaliland unakiuka moja kwa moja uhuru wa nchi hiyo.

Soma: Ethiopia yahofia ujumbe mpya wa amani wa Somalia 

Mchambuzi wa maswala ya Somalia Samira Gaid amesema mambo mawili yaliyopo mezani kwa wakati huu ni: Ethiopia ama ifute makubaliano kati yake na Somaliland au wanajeshi wake hawatakubaliwa tena kubakia kwenye ardhi ya Somalia.

Na pili ni Somalia kuwa karibu zaidi na Misri na kuikaribisha nchi hiyo kupitia ujumbe mpya wa kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Afrika na hatua hizo si jambo la kushangaza, kwa sababu ngoma za kuita vita zimekuwa zikipigwa kwa takriban miezi minane.

Rais wa Misri Abdel-Fattah al-Sisi Picha: THIBAULT CAMUS/AFP via Getty Images

Kwa upande wake Misri, nayo kwa miaka kadhaa imekuwa kwenye mvutano na Ethiopia kwa sababu ya ujenzi wa nchi hiyo wa bwawa kubwa la kuzalisha umeme kwenye mto Nile, Misri imelaani mpango wa Ethiopia na Somaliland.

Kwa mujibu wa Umoja wa Afrika kwenye taarifa yake ya mwezi Julai, Misri imejitolea kuchangia wanajeshi katika ujumbe mpya wa wanajeshi wa kulinda amani nchini Somalia.

Chanzo: /RTRE