1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaEthiopia

Ethiopia kuanza mazungumzo na kundi la waasi la Oromo

24 Aprili 2023

Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed, amesema serikali yake itaanzisha leo mazungumzo huko nchini Tanzania na kundi la waasi lililoko katika jimbo la Oromia, lenye watu wengi zaidi na linauzunguka mji mkuu, Addis Ababa.

Archiv I  Abiy Ahmed
Picha: Tiksa Negeri/REUTERS

Taarifa hiyo ya mazungumzo ya amani kati ya serikali ya Ethiopia na Jeshi la Ukombozi la Oromo, OLA ilitolewa siku ya Jumapili na waziri mkuu huyo ambaye alisema kuwa serikali na watu wa Ethiopia, wanayahitaji mno mazungumzo hayo. Abiy ametoa wito kwa wadau wote kuwajibika kikamilifu.  

Jeshi la OLA limekuwa likipambana na serikali ya shirikisho ya Ethiopia tangu lilipogawanyika mwaka 2018 na chama cha kihistoria cha Oromo Liberation Front (OLF) kilipoachana na mapambano ya kutumia silaha.

Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy AhmedPicha: Facebook.com/Office PM Ethiopia

Abiy alitoa kauli hiyo katika mkutano uliyozijumuisha pande zote kwenye mchakato wa amani wa Tigray ambao ulishuhudia makubaliano mnamo Novemba Pili, ambayo pia yalimaliza mzozo wa miaka miwili kati ya serikali ya shirikisho na mamlaka za uasi za kikanda.    

Abiy, wala OLA hawakutoa maelezo zaidi juu ya muundo wa mazungumzo hayo, na ni nani angelikuwa mpatanishi.

Soma pia: Abiy Ahmed atangaza uwezekano wa mazungumzo na waasi wa Oromo

OLA imethibitisha katika taarifa yake siku ya Jumatatu kuwa utawala wa Ethiopia umekubali masharti yao ya mazungumzo ya amani, ambayo ni pamoja na kumuhusisha mpatanishi huru na kuahidi kudumisha uwazi katika muda wote wa mchakato huo.

Taarifa hiyo ya OLA imeendelea kueleza kuwa hiyo ni hatua muhimu na nzuri kuelekea kuanzisha amani ya kudumu katika kanda hiyo, na kwamba tangu kuanza kwa mzozo huo, OLA imekuwa ikitoa wito wa mazungumzo ya amani mara kwa mara kama suluhu pekee, na inatia moyo kuona serikali hatimaye imefikia uamuzi kama huo.

Hii ni mara ya kwanza kwa serikali ya Ethiopia  kusema wazi kuwa itajadiliana na kundi la OLA, ambalo limekuwa mara kwa mara likipambana na serikali ya Ethiopia kwa miongo kadhaa.

Historia ya makundi ya uasi Oromia     

Kundi la watu wakisherehekea kurejea kwa kundi la OLF (15.09.2018) baada ya mabadiliko ya kisiasa nchini Ethiopia.Picha: Michael Tewelde/AFP

Mgawanyiko wa makundi ya waasi wa Oromia ulizua makundi kadhaa yenye silaha yaliyodai kuwa na umoja, lakini yenye mahusiano yasiyo thabiti.

Nguvu na uwezo wa kundi la OLA, iliyokadiriwa mwaka 2018 kuwa na maelfu ya wapiganaji, imeongezeka maradufu katika miaka ya hivi karibuni, ingawa wachambuzi wanaamini kuwa kundi hilo halina uratibu au silaha za kutosha ili kuwa kitisho cha wazi kwa serikali ya shirikisho ya Ethiopia.    

Eneo la Oromia limekuwa likikumbwa na mauaji ya kikabila katika miaka ya hivi karibuni yaliyoendeshwa na vikundi kadhaa visivyojulikana.

Soma pia:Abiy Ahmed aapa kuyavunja majeshi ya mikoa 

OLA imekuwa ikishutumiwa mara kwa mara na serikali ya Waziri Mkuu Abiy kwa kuhusika na mauaji hayo, lakini kundi hilo linaendelea kukanusha. Serikali inashutumiwa pia kwa kuendesha ukandamizaji kiholela ambao umechochea chuki ya watu wa Oromo dhidi ya serikali kuu.

Mwezi Februari, tume ya haki za binadamu iliyoteuliwa na serikali ilisema watu wasiopungua 50 waliuawa katika shambulio linalodhaniwa kutekelezwa na kundi la OLA.

Mwezi Oktoba mwaka jana, OLA na kikundi kingine cha Oromo viliilaumu serikali ya Ethiopia kwa mashambulizi ya anga na kusema yalisababisha vifo vya idadi kadhaa ya raia.

OLA imepinga pia kauli ya Abiy  ya kuwaita "Shene", wakisema jina hilo linawakilisha vibaya utambulisho na malengo yao.

OLA ni kikundi kilichopigwa marufuku na kilichojitenga na Oromo Liberation Front (OLF), ambacho ni chama cha upinzani kilichopigwa marufuku hapo awali na kilichorejea kutoka uhamishoni baada ya Abiy kuchukua madaraka mwaka 2018.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW