1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ethiopia: Makombora yarushwa kuelekea nchi jirani ya Eritrea

Zainab Aziz Mhariri: Amina Mjahid
29 Novemba 2020

Makombora kutoka mkoa wa kaskazini wa Tigray nchini Ethiopia yameulenga mji mkuu wa Eritrea, Asmara saa kadhaa baada ya Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed kutangaza kumalizika kwa operesheni ya kijeshi katika eneo hilo.

Karte Eritrea Djibouti DEU
Picha: DW

Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed alitangaza ushindi katika kampeni yake ya kijeshi dhidi ya chama tawala cha jimbo la Tigray, Tigray People's Liberation Front (TPLF). Ubalozi wa Merekani katika mji mkuu wa Eritrea, Asmara uliripoti mapema Jumapili juu ya milipuko sita iliyotokea jijini humo Jumamosi usiku.  

Hata hivyo ni vigumu kuthibitisha kama mji mkuu wa mkoa wa Tigray, Mekele umedhibitiwa na serikali ya shirikisho, ingawa msemaji wa jeshi la serikali ameliambia shirika la habari la AFP kwamba operesheni iliendelea vizuri.

Soma Zaidi:Abiy Ahmed: Jeshi la Ethiopia limechukua udhibiti wa Mekele

Mashambulio hayo ya makombora ni kwa mara ya tatu yanayoulenga mji mkuu wa Eritrea, Asmara tangu kuanza operesheni ya kijeshi hapo Novemba 4 dhidi ya utawala wa jimbo la Tgray katika nchi jirani ya Ethiopia, ingawa TPLF imedai kuhusika na shambulio la kwanza tu wiki mbili zilizopita.

TPLF imehalalisha mashambulio hayo kwa kuilaumu serikali kuu ya Ethiopia kwa kupokea msaada wa jeshi la Eritrea katika operesheni yake kwenye jimo la Tigray, madai ambayo serikali ya Ethiopia imeyakanusha.

Eritrea ni nchi mojawapo inayojiendehsa kwa usiri mkubwa ulimwenguni, na serikali mpaka sasa haijatoa tamko lolote kuhusiana na mashambulio hayo ya makombora.

Rais wa Eritrea Isaias AfwerkiPicha: Eritrea Minister of Information/Y.G. Meskel

Mawasiliano yalikatwa katika jimo la Tigray tangu mzozo ulipoanza, hali ambayo imesababisha ugumu katika kutathmini hali halisi ya mapigano makali ambapo mamia ya raia wamekufa na wengine maalfu wanakimbilia nchi jirani ya Sudan.

Waziri mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed amesema polisi wanaendeleza msako wa kuwakamata viongozi wa TPLF, ambao hawajulikani walipo. Kwa upande wake TPLF imeapa kuendeleza mapigano dhidi ya wanajeshi wa serikali kuu watakaokuwepo katika jimo la Tigray. Wachambuzi wameeleza wasiwasi kwamba mapigano hayo yanaweza kugeukia mbinu za uasi.

Vyanzo: AFP/DPA

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW