Ethiopia yaahidi kutekeleza makubaliano ya amani na Eritrea
6 Juni 2018Chama tawala kimesema Ethiopia imeamua kutekeleza makubaliano hayo ya amani ya Algiers yanayohusu mpaka wa Eritrea na Ethiopia bila ya masharti yoyote, kulingana na kituo cha televisheni ya taifa Fana. Taifa hilo limesema litafanya kazi kwa bidii kuyatekeleza makubaliano hayo.
Tangazo hilo linamaanisha Ethiopia inakubali uamuzi wa ugawaji wa mipaka wa makubaliano hayo ya Algiers wa mwaka 2000 ulioipa Eritrea haki ya kumiliki maeneo waliokuwa wakiyazozania ikiwa ni pamoja na mji wa Badme. Lakini hadi hivi sasa Ethiopia bado imeweka wanajeshi wake katika eneo hilo. Maelfu ya watu waliuawa wakati wa vita vya miaka miwili vilivyoanza mwaka 1998.
Aidha, mapema jana wabunge wa Ethiopia walipiga kura ya kuunga mkono kuondoa hali ya hatari iliyokuwa imetangazwa nchini humo. Wabunge wanane walikataa kupiga kura kabisa.
Hali hiyo ya hatari ya hivi karibuni iliwekwa katikati ya mwezi Februari baada ya kutokea maandamano makubwa dhidi ya serikali katika maeneo ya Oromia na Amhara.
Hatua za kukubali makubaliano hayo ya amani na Eritrea na kuondosha hali ya hatari ni mabadiliko muhimu ya hivi karibuni chini ya uongozi wa waziri mkuu mpya Abiy Ahmed, ambaye amezungumzia wazi juu ya haja ya kuleta mageuzi nchini humo.
Hali kadhalika, waziri mkuu huyo amewaachilia huru wafungwa wa kisiasa na kuanzisha mazungumzo na makundi ya upinzani tokea kuingia madarakani mwezi Aprili.
Uwekezaji binafsi wakaribishwa
Mbali na hayo, Ethiopia pia imesema jana kuwa shirika lake la simu linaloendeshwa na serikali pamoja na shirika la usafiri wa ndege yatakaribisha uwekezaji wa sekta binafsi. Ni sera muhimu ambayo inatarajiwa kupunguza udhibiti wa serikali katika uchumi wa nchi.
Taifa hilo la Afrika Mashariki lenye idadi ya watu wapatao milioni 100, linaongoza barani Afrika kwa kuwa na uchumi unaodhibitiwa na serikali.
Muungano tawala wa EPRDF, ambao umekuwa madarakani tokea 1991, kwa muda mrefu umekuwa ukiunga mkono uchumi unaodhibitiwa na serikali.
Lakini muungano huo umesema jana kwamba Ethiopia inahitaji mageuzi ya kiuchumi ili kupata ukuaji wa haraka na kuimarisha mauzo yake ya nje ya nchi.
Milango pia itafunguliwa kwa wawekezaji binafsi katika mashirika mengine yaliyo kwenye mikono ya serikali kama vile shirika la reli, kiwanda cha sukari, mahoteli na viwanda mbalimbali vya uzalishaji.
Abiy anatajwa kuwa chini ya shinikizo la kutimiza matarajio ya umma. Katika miezi miwili iliyopita amekuwa akitembelea maeneo mbalimbali ya Ethiopia akiahidi kushughulikia malalamiko ya raia kuhusu ukosefu wa haki za kisiasa na kiraia unaoshuhudiwa nchini humo.
Mwandishi: Yusra Buwayhid/rtre/dpa
Mhariri: Daniel Gakuba