1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ethiopia yatengeneza jukwaa lake la mtandao wa kijamii

23 Agosti 2021

Taasisi ya mawasiliano ya taifa nchini Ethiopia imesema, taifa hilo limeanza kuunda teknolojia mpya ya mtandao wa kijamii ili kutoa ushindani kwa mitandao ya kijamii ya  Facebook, Twitter na WhatsApp

WhatsApp - Instant-Messaging-Dienst
Picha: picture-alliance/N. Ansell

Tangu mwaka uliyopita Serikali ya Ethiopia imekuwa ikikosolewa kutokana na mgogoro kati ya jeshi lake dhidi vikosi vya chama cha ukombozi wa watu wa Tigray TPLF kinachodhibiti jimbo la Tigray Kaskazini mwa nchi hiyo.

Wafuasi wa pande zote mbili walianza kushambuliana kwa maneno kupitia mitandao ya kijamii. Kulingana na Mkurugenzi wa habari za usalama wa mtandaoni INSA Shumete Gizaw, serikali ya Ethiopia inataka mtandao wake wa kijamii kuchukua nafasi ya Facebook, Twitter, Whatsapp na Zoom.

Shumete ameishutumu facebook kwa  kufuta ujumbe  na kuzifungia akaunti za  baadhi ya watumiaji waliokuwa wakijaribu kuelezea hali halisi ya kile kilichokuwa kinaendelea nchini Ethiopia.

Upande mwingine mashirika ya kutetea haki za binaadamu, yameikosoa serikali ya Ethiopia,kwa  kufungia bila maelezo huduma za mitandaoni kupitia Facebook na WhatsApp mwaka mmoja uliyopita. serikali hadi sasa haijatoa tamko lolote kuhusu suala la kufungiwa  huduma hizo.

Facebook yakataa kutoa maoni juu ya mpango wa Ethiopia

Nembo ya mtandao wa kijamii wa FacebookPicha: Metin Aktas/AA/picture alliance

Msemaji wa mtandao wa Facebook Afrika, Kezia Anim-Addo alikataa kutoa maoni kuhusu mpango huo wa Ethiopia na hakuweza pia kusema lolote juu ya tuhuma zilizotolewa na Shumete.

Lakini mwezi Juni siku kadhaa kabla ya zoezi la uchaguzi wa kitaifa, Facebook ilisema ilifuta akaunti bandia  Ethiopia walizozifungamanisha na watu waliokuwa wakifanyia kazi shirika la  INSA linalosimamia na kufuatilia mawasiliano na intaneti nchini humo. Twitter haikutaka kutoa tamko juu ya teknolojia hiyo mpya ya Ethiopia  na mtandao wa Zoom kwa upande wake haukujibu  ombi la kuutaka utoe mtazamo wake kuhusu hilo.

Aidha mkurugenzi wa INSA- Shumete alikataa kutoa maelezo zaidi juu ya teknolojia hiyo mpya ya mawasiliano ya mtandao huku akisema nchi hiyo ina wataalamu wa kutosha kufanya kazi hiyo na kwamba haitoandika watu kutoka nje kuja kusaidia. Shumete pia amekataa kutaja muda wa kumalizika utengenezaji wa teknolojia hiyo lakini ameliambia shirika la habari la Reuters kwamba lengo lao la kuunda teknolojia yao wenyewe liko wazi na hasa pale mtu anapojiuliza ni kwanini unafikiri China inatumia mtandao wake yenyewe wa WeChat?

Ikumbukwe kwamba Teknolojia ya mtandao wa WeChat inamilikiwa na serikali ya china na inatumika sana nchini humo na inaangaliwa kama chombo muhimu kwa serikali kuwafuatilia watu wake.

Shumete amesema serikali inafanya kazi kubwa ya kutengeneza mtandao wake ili kuchukua nafasi ya  Facebook naTwitter, wakati majaribio yakiwa yameshafanyika ya mtandao utakaochukua nafasi ya WhatsApp na Zoom na kwamba mtandao huo utaanza kufanya kazi hivi karibuni.

Chanzo: Reuters

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW