Ethiopia yafuta mashitaka dhidi ya viongozi wa waasi wa TPLF
31 Machi 2023Serikali ya Ethiopia hapo jana imetangaza kuwaondolea mashtaka ya uhalifu viongozi wa Chama cha Ukombozi wa Watu wa Tigray TPLF, kama ilivyoainishwa katika mpango wa amani kaskazini mwa nchi hiyo.
Tangazo hilo lililotolewa na wizara ya sheria ya Ethiopia ni hatua ya hivi karibuni inayoonesha imani iliyoko katika mkataba huo wa amani.
Wiki iliyopita, serikali ya Ethiopia ilisema imemteua afisa mmoja mwandamizi wa TPLF kuwa mkuu wa utawala wa mpito wa Tigray. Uteuzi huo ulifanyika siku moja tu baada ya bunge la nchi hiyo kuliondoa kundi la TPLF katika orodha rasmi ya makundi ya kigaidi.
Mgogoro wa Tigray ulianza Novemba 2020 pale Waziri Mkuu Abiy Ahmed alipoyatuma majeshi Tigray kuuangusha uongozi wa TPLF akiwashutumu wapiganaji wake kwa kushambulia kambi za kijeshi za shirikisho.