Ethiopia yailaumu TPLF kwa kutoshirikiana kutafuta amani
19 Agosti 2022Serikali ya Ethiopia imekituhumu Chama cha Ukombozi cha Watu wa Tigray (TPLF) kwa kutoonesha ushirikiano katika kufanikisha mazungumzo ya amani, yenye lengo la kumaliza vita vilivyodumu kwa miezi 21, vya kaskazini mwa taifa hilo.
Mnamo Alhamisi, Msemaji wa Waziri Mkuu, Abiy Ahmed, Abiy Billene Seyoum, alisema serikali inaendelea kutoa wito wa kutatuliwa kwa amani mzozo huo licha ya kuwa hakuna hamasa hata kidogo ya kuonesha maslahi ya amani kwa upande wa TPLF.
Akizungumza na waandishi wa habari msemaji huyo alisema "Kama TPLF inajali kwa dhati ustawi wa Waethiopia katika eneo la Tigray wanapaswa kushiriki mazungumzo badala ya kutafuta visingizio vya kuepusha amani."
Serikali ya Waziri Mkuu Abiy Ahmed na Chama cha Ukombozi cha Watu wa Tigray (TPLF) katika wiki za hivi karibuni wameibua matarajio ya kufanyika mazungumzo ya amani, lakini bado kumekuwa na vikwazo, huku pande zote mbili zikilaumiana kwa mkwamo huo.