Ethiopia yataka Eritrea iondoe vikosi kwenye eneo lake
8 Februari 2026
Waziri wa mambo ya nje wa Ethiopia Gedion Timothewos kupitia barua yake ya jana Jumamosi amemuambia mwenzake wa Erithrea kuwa, matukio ya siku kadhaa zilizopita yanaashiria kuwa serikali ya Asmara imechagua njia inayochochea mvutano. Barua hiyo imetaka ushirikiano wowote kati ya Eritrea na waasi usitishwe haraka.
Bado diplomasia inaweza kutumika
Hata hivyo Timothewos amesema bado anaamini kuwa hali ya ghasia na kutokuaminiana inaweza kumalizwa kidiplomasia. Hadi sasa Eritrea haijajibu chochote kuhusu shutuma hizo. Eritrea ilipata uhuru kutoka kwa Ethiopia mwaka 1993. Nchi hizo zilipigana vita vikali vya mpaka vilivyowauwa maelfu ya watu mwaka 1998 hadi 2000.
Nchi hizo zilishirikiana kwa muda, wakati wa mzozo wa Tigray zilipokuwa zikipambana na vikosi vya eneo hilo. Mahusiano yalizorota baada ya Ethiopia kusaini makubaliano ya amani ambayo hayakuihusisha Eritrea mwaka 2022.