Ethiopia yaishutumu Eritrea, TPLF kwa kutaka kuanzisha vita
8 Oktoba 2025
Waziri wa Mambo ya Nje wa Ethiopia Gedion Timothewos amemuandikia barua Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa antonio Guterres "ushirikiano kati ya serikali ya Eritrea na TPLF umeonekana wazi zaidi katika miezi ya hivi karibuni,” akiongeza kuwa "kundi la wanamgambo wa TPLF na serikali ya Eritrea wanaandaa vita dhidi ya Ethiopia.”
Kwa mujibu wa Addis Ababa, serikali ya Eritrea na TPLF zinahusika katika kufadhili, kuhamasisha na kuelekeza makundi ya waasi katika eneo la Amhara, ambako jeshi la shirikisho limekuwa likipambana na wapiganaji kwa miaka kadhaa. Hadi sasa, Waziri wa Habari wa Eritrea, Yemane Ghebremeskel na viongozi wa TPLF hawajatoa majibu kuhusu tuhuma hizo.
Uhusiano wa Ethiopia na Eritrea wazidi kuzorota
Uhusiano kati ya nchi hizo mbili umekuwa ukidorora kwa miezi kadhaa zaidi ya miaka 30 tangu Eritrea ipate uhuru wake mwaka 1993 baada ya vita vya muda mrefu vya kujitenga na Ethiopia. Vita vya mpaka vilivyofuatia kati ya mwaka 1998 na 2000 vilisababisha vifo vya maelfu ya watu na kuacha alama ya chuki ya kudumu kati ya mataifa hayo jirani.
Mnamo mwaka 2018, matumaini mapya yalijitokeza baada ya Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed kuiingia madarakani na kusaini makubaliano ya amani na Rais Isaias Afwerki wa Eritrea, hatua iliyopokelewa kwa shangwe duniani na kumpatia Abiy Ahmed Tuzo ya Amani ya Nobel mwaka 2019.
Hata hivyo, uhusiano huo uliharibika tena baada ya Eritrea kutuma wanajeshi wake kuisaidia Ethiopia wakati wa vita vya Tigray kati ya mwaka 2020 na 2022 — vita vilivyogharimu maisha ya takribani watu 600,000 kwa mujibu wa makadirio ya Umoja wa Afrika.
Baada ya vita hivyo kumalizika hali ya uhusiano imezidi kuwa baridi huku Asmara ikiilaumu Addis Ababa kwa kujaribu kudai ufikiaji wa bahari kupitia bandari ya Assab iliyoko kusini mashariki mwa Eritrea. Ethiopia, nchi isiyo na bandari, imekuwa ikisisitiza kwamba inahitaji kufufua haki ya kufikia Bahari ya Shamu, jambo ambalo Eritrea inaliona kama tishio kwa uhuru wake.
Ethiopia inataka 'mazungumzo ya dhati' na Eritrea
Katika barua yake kwa Umoja wa Mataifa, Waziri Gedion alisisitiza kuwa Addis Ababa "inataka kufanya mazungumzo ya dhati kwa nia njema na serikali ya Eritrea,” lakini akaishutumu Asmara kwa "kutumia madai ya tishio la bahari kama kisingizio cha mipango yake ovu dhidi ya Ethiopia.”
Mwezi Juni, ripoti ya shirika la ufuatiliaji la Marekani The Sentry ilidai kuwa Eritrea inaendelea kujenga upya jeshi lake na kuchochea mivutano katika ukanda wa Pembe ya Afrika. Lakini Waziri wa Habari wa Eritrea, Ghebremeskel, alikanusha madai hayo na kusema "mvutano mpya wa kikanda unasababishwa na sera za Ethiopia.”
Wakati hayo yakijiri, Eritrea — yenye idadi ya watu takribani milioni 3.5 — imekuwa ikizidisha ushirikiano wake wa kijeshi na Misri, taifa ambalo pia lina uhusiano uliozorota na Ethiopia kutokana na mzozo wa Bwawa la Umeme la Renaissance (GERD). Wataalamu wa kikanda wanaonya kuwa mvutano huu mpya unaweza kuirudisha Pembe ya Afrika katika hatari ya mzunguko mwingine wa vita vya mpaka.