1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ethiopia yaitaka Marekani kuacha kusambaza taarifa za uwongo

Admin.WagnerD26 Novemba 2021

Serikali ya Ethiopia Alhamisi imeionya Marekani kuacha kutangaza taarifa za uwongo, huku mapigano ya mwaka mzima nchini humo yakiwa yanaunyemelea mji mkuu wa Addis Ababa.

Äthiopien Konflikt mit Tigray
Picha: AMANUEL SILESHI/AFP/Getty Images

Msemaji wa serikali Kebele Desisa amesema vita vya Ethiopia havipambani tu na vikosi vya eneo la nchini hiyo la Tigray, bali pia mataifa ya Magharibi yenye nguvu. Aidha ameitaka Marekani kusita kusambaza taarifa za uwongo zinazoikashifu Ethiopia.

Aliyasema hayo kufuatia onyo la ubalozi wa Marekani la kuwataka raia wake nchini humo kuondoka kwani kuna uwezekano wa kutokea shambulio la kigaidi. Halikadhalika Marekani imesema hakutakuwapo usaidizi kama ulitolewa wakati wa ghasia za Afghanistan iwapo mapigano yataingia mji mkuu wa Addis Ababa.

Baadhi ya Waethiopia walikasirishwa na matamshi hayo ya ubalozi wa Marekani. Na mapema jana waliandamana nje ya ubalozi huo mjini Addis Ababa, wakipinga uingiliaji kati wa nchi za Magharibi katika mambo ya ndani ya Ethiopia,

Marekani pia imeonya siku ya Jumatano kuwa hakuna suluhu la kijeshi linaloweza kutuliza vita hivyo vya wenyewe kwa wenyewe, badala yake imeshauri kwamba mazungumzo ya kidiplomasia ndiyo njia pekee itakayoleta amani.

Marekani ilisema hayo baada ya vyombo vya habari nchini Ethiopia kutangaza kwamba tayari Waziri Mkuu Abiy Ahmed yupo uwanja wa vita ameungana na vikosi vyake vya kijeshi.

Abiy asema anapambana pia na ushawishi wa Magharibi

Sio Marekani pekee, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres pia alitoa wito wa kusitishwa kwa mapigano mara moja nchini Ethiopia.

"Mchakato wa kutafuta amani wa Colombia unanitia moyo kutoa wito kwa wahusika wakuu wa mzozo nwa chini Ethiopia wa kusitisha mapigano bila ya masharti na mara moja, ili kuiokoa nchi na kuruhusu mazungumzo yafanyike kati ya Waethiopia," amesema Antonio Guterres.

Mzozo wa Ethiopia na TigrayPicha: AP/picture alliance

Waziri Mkuu Abiy Ahmed, alitangaza wiki hii kuwa anakwenda vitani kupambana na viongozi wa kundi la TPLF la eneo la Tigray, ambao kwa muda mrefu walikuwa wakiidhibiti serikali ya kitaifa, kabla ya kupoteza ushawishi huo kufuatia mzozo wa kisiasa.

Lakini hivi sasa amebadilisha kauli yake, na kuyatolea wito mataifa mengine ya Kiafrika kumsaidia katika mapambano hayo dhidi ya uingiliaji kati wa nchi za Magharibi.

Maelfu ya watu wameuawa katika mzozo huo uliozuka mnamo mwezi Novemba 2020, na karibu watu nusu milioni wa eneo la Tigray wanakabiliwa na baa la njaa huku njia za kupitisha misaada zikiwa zimefungwa na vikosi vya serikali kwa miezi kadhaa.

Soma zaidi: UN yatoa fedha za msaada wa dharura Ethiopia

Vikosi vya Tigray vimesema vimekuwa vikiishinikiza serikali ya Abiy kufungua njia hizo ili kupitishwe misaada ya kiutu, lakini pia inamtaka waziri mkuu ajiuzulu.

Mapema mwaka huu, serikali ya Ethiopia imelitangaza kundi hilo la Tigray kuwa ni la kigaidi, hali inayokwamisha juhudi za upatanishi zinazojaribu kufanywa na Marekani pamoja na Umoja wa Afrika ili kusitisha mapigano hayo.

Vyanzo: (ap, afp, rte)

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW