1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tume ya majadiliano ya kitaifa kuundwa Ethiopia

30 Desemba 2021

Wabunge wa Ethiopia wamepitisha msuada utakaoidhinisha kuundwa kwa tume ya mazungumzo ya kitaifa kufuatia shinikizo la kimataifa la kuwepo kwa mazungumzo hayo yanayonuiwa kumaliza vita vya miezi 13 katika jimbo la Tigray

Äthiopien Premierminister Abiy Ahmed stellt im Parlament sein neues Kabinett vor
Picha: Ethiopian Prime Minister Office

Bunge la shirikisho lilipiga kura kuidhinisha msuwada huo kwa kura 287 huku kura 13 zikiupinga na moja kutopigwa kabisa.  Kuundwa kwa tume hiyo kutafungua njia ya majadiliano ya kitaifa  na kukuza uaminifu wa taifa.

Serikali ya Waziri Mkuu Abiy Ahmed iliahidi kuunda tume hiyo ili kuwa na mahala pa kujadili masuala yanayoleta utata. Hata hivyo tume hiyo kwa sasa haitolijumuisha kundi la TPLF wala Jeshi la ukombozi la Oromo katika majadiliano. Makundi yote mawili yanapambana na jeshi la Ethiopia na yalitangazwa kuwa makundi ya kigaidi na serikali ya taifa hilo la Afrika Mashariki.

Lakini kuundwa kwa tume huenda kukawa ni juhudi ya Ethiopia kujibu shinikizo kutoka kwa jamii ya kimataifa kutaka mapigano yasitishwe na mazungumzo ya kutafuta suluhu ya kudumu wa mvutano uliopo.

Tsedale Lemma mkurugenzi wa chombo kimoja cha habari nchini Ethiopia amesema wakati Jamii ya kimataifa ilipopendekeza kuwepo kwa mazungumzo ya kitaifa ilimaanisha kujumuishwa kwa makundi yote kuwa sehemu ya mchakato wa upatikanaji wa amani, lakini kwa sasa serikali ya Ethiopia ina sera ya kutojadili chochote na makundi yaliojihami.

Tsedale Lemma amesema iwapo hilo litafanyika, basi itakuwa ni juhudi ya serikali kuunda tume ambayo haina nia yoyote ya kutatua mgogoro wa kisiasa unaoikumba nchi hiyo.

Ethiopia: Mataifa ya Magharibi iache kuingilia mambo yake ya ndani

Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed Picha: Office of the Prime Minister Ethiopia/UPI Photo/Newscom/picture alliance

Huku hayo yakiarifiwa ubalozi wa Marekani, Ethiopia unaendelea kuwatolea wito raia wake wanaotaka kuondoka nchini humo kufanya hivyo mara moja.

Awali Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani Anthony Blinken alizungumza na rais wa Kenya Uhuru Kenyatta kuhusu hali ya kisiasa nchini Ethiopia na kukubaliana kuhusu umuhimu wa kukomesha uhasama, kutoa nafasi ya kufikiwa kwa huduma za kiutu, kusitishwa kwa ukiukwaji wa haki za binaadamu na kutoa nafasi ya kutafuta suluhu ya mgogoro uliopo.

soma zaidi: Ethiopia yaishutumu Marekani kwa taarifa zenye kubomoa

Kwa upande wao maafisa wa serikali wameendelea kushikilia msimamo wao kwamba Marekani na mataifa mengine ya Magharibi wanaingilia mambo ya ndani ya taifa hilo.

Vita vya nchini Ethiopia vinasemekana kusababisha vifo vya maelfu ya watu huku mamilioni ya wengine wakikosa makaazi na kuwaweka wengi katika hatari ya kukabiliwa na baa la njaa katika jimbo la Tigray hii ikiwa ni kulingana na makundi ya misaada. Pande zote mbili katika vita hivyo zimeshutumiwa kutekeleza uhalifu, mauaji na unyanyasaji wa kingono.

Chanzo: afp/ap