Ethiopia yarejesha ndege za Boeing 737 MAX
1 Februari 2022Kupitia taarifa iliyotolewa leo, shirika hilo la ndege limesema uamuzi wa kuanza kutumia tena ndege chapa737 MAX umechukuliwa baada ya ukaguzi wa kina uliofanywa na wasimamizi wa usafiri wa anga nchini Marekani, Umoja wa Ulaya, China na Ethiopia kwenyewe.
Katika safari ya kwanza ndege ya shirika hilo iliruka kwenye anga ya Ethiopia kwa muda saa nne ikiwa imewabeba wawakilishi wa shirika, wale kutoka kampuni ya Boeing na balozi wa Marekani nchini Ethiopia.
Soma Zaidi:Rubani wa ndege ya Ethiopia iliyoanguka alifuata maelekezo: Ripoti
Ajali ya mwezi Machi mwaka 2019 iliyohusisha ndege ya Ethiopia chapa 737 MAX ilisababisha mataifa duniani kusitisha matumizi ya aina hiyo ya ndege baada ya taharuki kwamba huenda mifumo yake ya kiufundi ilikuwa na hitilafu.
Kwenye taarifa kwa shirika la habari la AFP wiki hii, shirika hilo la ndege lilisema uamuzi wa kurejesha safari za ndege hizo za 737 MAX baada ya uthibitisho wa kina kutoka kwa wasimamizi nchini Marekani, Umoja wa Ulaya, China na Ethiopia kwenyewe. Aidha lilitoa pia orodha ya mashirika mwengine 35 ambayo pia yameanza kuzitumia tena ndege hizo.
Safari ya Jumanne hii, awali ilipangwa kuelekea Kilimanjaro nchini Tanzania, lakini hali mbaya ya hewa ilisababisha kubadilisha safari hiyo. Ndege hiyo ilipita karibu na Mlima Zuqualla, kuelekea Milima ya Bale kabla ya kurejea Addis Ababa.
Lakini kwa wale waliopoteza wapendwa wao miaka mitatu iliyopita kwenye ajali hiyo hata hivyo wamesema siku hii si ya furaha kwao. Familia za wahanga wa ndege 302 iliyoanguka, katika ajali mbaya kabisa kutokea nchini Ethiopia walitokea katika mataifa zaidi ya 30, lakini wengi wao walikuwa ni raia wa Kenya.
Rais wa familia hizo zawahanga hao Virginie Fricaudet alisema kurejeshwa kwa safari hizo kutarejesha maumivu makubwa kwake. Fricaudet, alipoteza kaka yake kwenye ajali hiyo.
Mashirika: AFPE