1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ethiopia yasema ripoti ya Umoja wa Mataifa ni ya kibaguzi

21 Septemba 2022

Ethiopia imeikosoa na kuikataa ripoti ya wachunguzi wa Umoja wa Mataifa, iliyoituhumu kwamba huenda ikawa inatekeleza uhalifu dhidi ya binaadamu katika eneo la Tigray linalokumbwa na vita.

Äthiopien Premierminister Abiy Ahmed stellt im Parlament sein neues Kabinett vor
Picha: Ethiopian Prime Minister Office

Kulingana na tume ya wataalamu wa haki za binaadamu kuhusu Ethiopia, imepata ushahidi wa ukiukwaji mkubwa wa haki za binaadamu unaofanywa na pande zote tangu vita vilipozuka katika jimbo la Tigray takriban miaka miwili iliyopita.

Pande hizo ni pamoja na serikali ya Waziri Mkuu Abiy Ahmed ambaye pia ni mshindi wa tuzo ya Nobeli na washirika  wake ambao wamekuwa wakisababisha mateso makubwa kwa kukataa usaidizi ufike Tigray eneo lililo na idadi ya watu milioni sita.

soma zaidi: Watu 10 wauawa katika mashambulizi ya anga Tigray

Kaari Betty Murungi, moja ya wataalamu wa tume hiyo, amesema kuwanyima watu chakula, dawa, na huduma nyengine muhimu kunasababisha madhara makubwa kwa raia. Amesema hatua kama hizo zinawafanya waamini kuwa kuna uhalifu mkubwa dhidi ya binaadamu katika eneo hilo. Amesema pia wanasababu za kutosha kuamini kwamba serikali ya Ethiopia, inatumia njaa kama silaha ya vita.

Ethiopia yasema ripoti iliyotolewa inalalia upande mmoja

Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed Picha: Minasse Wondimu Hailu/AA/picture alliance

Hata hivyo mwakilishi Maalum wa Ethiopia katika Umoja wa Mataifa mjini Geneva Zenebe Kebede, amesema tume hiyo imeshinikizwa kisiasa na kilichoandikwa kinalalia upande mmoja. Akizungumza na shirika la habari la AFP Kebede amesema hakuna hata siku moja serikali ya Ethiopia ilitumia misaada ya kiutu kama silaha ya vita, huku akisema ripoti hiyo ni ya "kipuuzi" na hawana budi kuikataa.

Kumi wauwawa katika shambulio Ethiopia

Mwakilishi huyo Maalum wa Ethiopia katika Umoja wa Mataifa pia amesema wachunguzi wamepuzilia mbali ukatili uliofanywa na kundi la TPLF ambalo Adis Ababa inalichukulia kama kundi la kigaidi lililoiongoza Ethiopia kwa miongo kadhaa kabla ya Abiy kuingia madarakani mwaka 2018.

Mapigano kati ya vikosi vya serikali, washirika wake na waasi wa TPLF yalianza upya mwezi Agosti baada ya miezi mitano ya utulivu katika jimbo la Tigray. Kurejea kwa mapigano kumekuja baada ya juhudi za kidiplomasia kuongezeka kwa nia ya kujaribu kutafuta amani katika mzozo wa takriban miaka miwili katika taifa hilo la Afrika.

Wakati hayo yakiarifiwa mwezi huu kundi la TPLF lilisema iko tayari kushiriki mazungumzo ya amani yatakayosimamiwa na Umoja wa Afrika likiondoa kizuizi kilichokuwepo cha kukataa kuzungumza na serikali ya Abiy Ahmed. Lakini mapigano yameendelea kushuhudiwa wiki kadhaa baada ya tangazo hilo huku mashambulizi ya angani yakishuhudiwa katika eneo la Tigray na washirika wa Abiy Eritrea wakionekana kutuma wanajeshi wake kuungana na jeshi la Abiy katika mapigano hayo.

Chanzo: afp